Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amezitaka taasisi zinazosimamia maendeleo ya Sekta ya Maji mkoani humo kuboresha huduma hiyo kwa wananchi ili kuondoa kero ya upatikanaji wa maji pungufu kwenye jamii.
Mhe. Malima amebainisha hayo leo Oktoba 25, 2022 wakati wa kikao kilichowakutanisha Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) na Mamlaka ya Huduma za Maji mjini Sengerema (SEUWASA) kufanya tathmini ya Maendeleo ya Miradi ya Maji Mkoani humo.
Mhe. Malima amesema kufuatia kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya huduma duni ya Upatikajai wa Maji wakati wa ziara ya Mhe. Abdulrahman Kinana (Makamu Mwenyekiti CCM Bara) Mkoani humo, imemsukuma kuziangalia kwa karibu taasisi zinazoshughulika na Maji ili kuhakikisha uzalishaji wa unaboreshwa mara moja.
Vilevile, ameagiza umakini na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ili kuondoa upotevu wa Maji uliofikia hadi asilimia 32 kwenye Mradi Mkubwa wa chanzo cha Kapripoint wenye uwezo wa kuzalisha lita Milioni 90 kwa siku lakini wanazalisha pungufu na kusababisha maeneo mengi ya wakazi wa Mji wa Mwanza kukosa maji ya kutosha.
Mhandisi Leonard Msenyele, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA akiambatana na wakandarasi na wafadhili wa mradi mkubwa wa Maji wa Butimba unaotarajia kuzalisha Lita Milioni 48 kwa siku amesema ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na kwamba wananchi watapata huduma iliyoboreshwa kwa wakati kadiri ya mkataba na kwamba mradi huo utaongeza huduma hiyo kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Salim Lossindilo amefafanua kuwa kuna tatizo la uchakavu wa mitambo linalokadiriwa kuhitaji Tshs Bilioni tatu ili kuondoa tatizo hilo na kwamba wanaendelea na jitihada za kupata pampu zitakazosaidia kuongeza nguvu kwenye vituo vya usambazaji vya Mabatini, Kona ya Bwiru na Nyegezi ili wananchi wanaoishi pembezoni wapate maji ya kutosha.
"Tatizo la Mji wa Mwanza Mkuu wa Mkoa ni kwamba upo kama bakuli kijografia, yaani usambazaji wa maji unakua mgumu sana kwa wananchi wanaoishi pembezoni na kwenye maeneo ya miinuko na hali hii tutaiondoa kwa kuboresha Miundombinu yetu kuwa imara zaidi wakati wote tofauti na hivyo wakazi wanaoishi kwenye maeneo tambarare na chini watanufaika zaidi." Amefafanua Mhandisi Lussindilo.
Amefafanua kuwa lengo la ukarabati huo ni kuhakikisha wanajaza matanki ya pembezoni kama Nyashana ambalo sasahivi linaingizwa maji kwa asilimia 50 tu na kwamba baada ya kupata mitambo hiyo huduma ya maji kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo yenye miinuko itaimarika kwani uzalishaji na usambazaji utaongezeka.
Meneja wa Ruwasa Mkoa Mhandisi Exaud Humbo amesema pamoja na kutekeleza miradi ya zaidi ya Bilioni 112 kwa mwakq 2022/23 wana changamoto ya Msamaha wa Kodi hali inayopelekea Miradi kuchelewa kuanza taratibu za manunuzi ambapo kati ya Miradi 29 ni sita tu imepata msamaha na kwamba kumekua na tatizo la wakandarasi kuzembea kazi.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal amefafanua kuwa Wizara ya Ujenzi na Mfuko wa Barabara wameshatoa zaidi ya Bilioni 10 kwa ajili ya Ujenzi wa Daraja la Simiyu lililopo Magu ili kuimarisha mawasiliano kwenye eneo hilo ambalo wakazi wake wanatumia daraja jembamba lililojengwa miaka mingi iliyopita na kwamba taratibu za utekelezaji zimeanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.