Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Desemba 16, 2025 amefanya kikao kifupi na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Mhe. Dkt. Jafar Rajab Seif, ambaye yupo mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya sekta ya afya katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kimejadili maendeleo ya huduma za afya katika mkoa huo, na kujadili mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na changamoto zinazokabiliwa na sekta hiyo.

Mhe. Dkt. Rajab Seif amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu katika kuhakikisha kwamba miradi ya afya inatekelezwa kwa ufanisi na inawanufaisha wananchi.

“Ziara yangu hapa Mwanza ni sehemu ya juhudi zetu za kuhakikisha kwamba huduma za afya zinaboreshwa na zinazifikia jamii kwa wakati. Tutaendelea kutoa kipaumbele katika maeneo ya afya ili wananchi wa Mwanza na maeneo mengine ya nchi wafaidike na huduma bora,” amesema Mhe. Dkt. Rajab Seif.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mtanda ameeleza kuridhishwa kwake na hatua ambazo tayari zimechukuliwa katika kuboresha huduma za afya katika mkoa wake.

Aidha amemshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kutembelea Mkoa huo na kuahidi kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya afya.

Ziara ya Mhe. Dkt. Jafar Rajab Seif imejumuisha ukaguzi wa vituo vya afya na hospitali katika wilaya za Ilemela na Nyamagana, ambapo amekutana na viongozi wa sekta ya afya pamoja na watumishi wa afya kwa lengo la kubaini changamoto na kujadiliana kuhusu njia za kutatua matatizo yanayojitokeza katika utoaji wa huduma.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.