RC MTANDA AHIMIZA ULIPAJI KODI, UWAJIBIKAJI NA AMANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda amewataka viongozi wa Chama na Serikali kuhimiza na kusimamia ulipaji kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Ametoa agizo hilo leo Disemba 24, 2024 wakati akihitimisha kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huku akisisitiza kuwa ili serikali iweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwaletea maendeleo ni lazima iwe na fedha.
"Machafuko tunayo yashuhudia hivi sasa ulimwenguni baadhi yanatokana na hasira za wananchi kukosa huduma za msingi huku Serikali ikikosa fedha kutokana na kushindwa kukusanya kodi", Mhe. Mtanda.
Aidha, amewaomba viongozi kushirikiana kuhakikisha nidhamu ya ulipaji kodi inakuwepo na Serikali kuendelea na mkakati ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Akizungumza kuhusu uwajibikaji Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watumishi kuweka mbele nidhamu ya uwajibikaji kwa wananchi na kuepukana na vitendo vya rushwa.
"Viongozi wote mliopo hapa mkiwemo wakuu wa Wilaya na Taasisi kasimamieni hili msimuonee mtu aibu kumchukulia hatua, wananchi wana Imani na Serikali hii ya kuwapa huduma bora",amesisitiza Mtanda wakati wa kuhitimisha kikao hicho.
Hali kadhalika, amehimiza amani na hasa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuwataka wananchi kuwa watulivu na kuepukana na aina yoyote ya uvunjivu wa amani huku dola likiwa makini wakati wote kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.
Katibu Tawala Mkoa wa
Mwanza Ndg. Balandya Elikana akijibu hoja ya mbunge wa Ilemela Mhe. Anjelina Mabula kuhusu ulipwaji wa fidia kaya 300,000 waliopisha maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege, amesema mchakato wote umekamilika kinachosubiriwa ni mrejesho kutoka mamlaka husika.
Kikao hicho cha Kamati ya Ushauri Mkoa kimepokea hoja ya Jimbo la Magu kugawanywa sehemu mbili na kuwepo Jimbo lingine la Sanjo kutokana na ukubwa na idadi ya wananchi zaidi ya laki nne huku hoja ya Jimbo la Sengerema kugawanywa na kuwepo na Jimbo la Karumo likitolewa maelekezo ya kufanyika kikao cha kitaalamu kabla ya kuwasilishwa kikao kijacho cha RCC.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.