Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesisitiza kuwa malezi bora ya mtoto hayawezi kufanikishwa na mzazi mmoja pekee, akibainisha kuwa ushirikiano wa karibu kati ya baba na mama ni nguzo muhimu katika kuhakikisha makuzi ya mtoto mwenye maadili, ujasiri na mafanikio ya baadaye.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo Septemba 19, 2025 alipokuwa katika Mahafali ya Kwanza ya Darasa la Saba na maonesho ya sayansi na ubunifu katika shule ya NEBRIX iliyopo Mtaa wa Chabakima Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa changamoto nyingi zinazowakumba watoto wa kizazi hiki zinachangiwa na ukosefu wa mshikamano wa kimalezi kati ya wazazi wawili, hali inayowafanya watoto kulelewa katika mazingira yasiyo na mwongozo thabiti.
“Siku hizi eti kuna Wazazi wanajiita single mothers, uongo mtupu, malezi ni ya wazazi wote wawili”.
Lakini pia Wazazi wa Kiume wamekuwa na shughuli nyingi wakisingizia wanatafuta pesa, sasa unakuta hawaweki dhamana ya kuwa karibu na watoto na mwisho wa siku fedha hawapati na ukaribu wa watoto haupo. Amesema Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Mtanda ameeleza ni lazima Wazazi wote wawili kushirikiana katika kufuatilia mienendo na tabia za watoto ili kuwajengea msingi imara wa maisha yao ya baadae na kutatua changamoto zao wanapokumbana nazo kwa haraka ili wasikumbane na vishawishi.
“Mkiwa karibu na Watoto wenu mnaleta bondi, msipofanya hivyo upendo hauji, na ndio maana Wazazi wengi wanatekelezwa baada ya watoto wao kufanikiwa”. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo pia kuwataka Wazazi/Walezi kuhakikisha wanashiriki katika shughuli za uchaguzi mkuu kuanzia kampeni mpaka kushiriki zoezi la upigaji kura ifikapo Oktoba 29, 2025.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.