RC MTANDA AWATAKA PAMBA JIJI KUJA NA MATOKEO MAZURI LALA SALAMA YA LIGI KUU
Wakati filimbi ya lala salama ya ligi kuu ya NBC imepulizwa timu ya Pamba Jiji FC imetakiwa kuja na matokeo mazuri dimbani baada ya kufanyiwa maboresho ya kiufundi ikiwemo ingizo la wachezaji wapya na kuondolewa wale walioonekana ni mzigo kwa timu.
Rai hiyo imetolewa leo Januari 29, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni mlezi wa Pamba Jiji FC Mhe.Said Mtanda wakati wa hafla fupi ya chakula cha jioni aliyowaandalia timu hiyo kwenye ukumbi wa Gadh Hall na kusisitiza hakutakuwa na simile ya kuchukua maamuzi magumu itakapo bainika muhusika yoyote anaonesha dalili za kuiangamiza timu.
"Nawaomba katika hili tuelewane vizuri uongozi umetumia gharama kubwa ya kuiboresha timu wale tuliowaona siyo msaada kwa timu na kujiona wao ni wakubwa wa kuliko Pamba Jiji tumewaondoa,nawataka muanze kujitambua kwa kujituma uwanjani ili malengo yetu ya kubaki ligi kuu yatimie,"amesisitiza Mtanda wakati akizungumza na wachezaji na dawati zima la ufundi la timu hiyo.
Mtanda ambaye ni mpenda soka kindakindaki amekemea vikali baadhi ya wachezaji wanaojiingiza katika michezo ya kamali na kusema huo ni utovu wa nidhamu usiyovumilika na hatua za kinidhamu zitamkuta yoyote atakaye bainika.
"Tayari kuna mmoja wenu nimempa onyo kali baada ya kumgundua kujihusisha na huo mchezo wa kijinga,nina uwezo wa hali ya juu wa kuwabaini narudia tena kuwaonya wacheni na wekeni mkazo uwanjani," mkuu wa Mkoa.
Aidha amelitaka pia dawati la ufundi chini ya kocha wake Freddy Felix Minziro kuwa chachu ya kufanya vizuri kwa timu hiyo kwani hata wao hawana uhakika wa kubaki salama endapo watakwenda kinyume na makubaliano yao kwenye mkataba.
Katika usajili wa dirisha dogo uliofanywa na uongozi wa timu hiyo kwa ushauri wa kocha Minziro miongoni mwa wachezaji wapya ni pamoja na mshambuliaji Deus Kaseke.
Pamba Jiji FC iliyopo nafasi ya 14 na mtaji wa ponti 12 kibindoni itashuka dimbani Februari 5 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri kupepetana na wenyeji wao Dodoma Jiji FC ambao katika mzunguko wa kwanza walitoshana nguvu ya bila kufungana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.