Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa Vijana waliomaliza Vyuo Vikuu, Kati na Ufundi kutafuta fursa sahihi pale wanapomaliza elimu ya vyuo na kuacha tabia ya kulalamika kwani jamii ya sasa inahitaji vijana wenye uwezo wa kutatua matatizo yanayoikabili jamii.

Mhe. Mtanda amesema matamanio ya Taifa ni kuona vijana wake wakiwa ni watu wenye uwezo wa kuzalisha mali kwa maslahi mapana ya maendeleo ya taifa kupitia fursa na uzoefu wanaopewa kutoka katika Taasisi za Umma na Binafsi.

Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo mapema leo Desemba 06, 2025 wakati alipokuwa kaifungua Kongamano la Fursa lililowakutanisha Vijana waliomaliza Vyuo mbalimbali Waishio Mkoani Mwanza katika ukumbi wa Kwatunza uliopo Wilayani Ilemela.

Aidha, Mhe. Mtanda amesema kuwa vijana wanapaswa kupata taarifa sahihi zihusuzo fursa mbalimbali ili ziwawezeshe kujiondoa kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika nyaza zote za kimaisha kwani upatikanaji wa taarifa sahihi ndio chachu ya hamasa na kujia ukweli wa upatikanaji wa fursa.

Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa idadi kubwa kwa sasa ya vijana hapa nchini ni vijana walio wasomi hivyo serikali inao wajibu wa kutengeneza mazingira wezeshi kupitia sekta binafsi ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa za ajira.

Mkuu wa Mkoa amesema pia kongamano hilo limelenga kunadi fursa ziliopo katika sekta binafsi kwani kupitia sekta hizo zitasaidia kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi wanaomaliza vyuo hapa nchini.

“Kupitia sekta hizo vijana watapa fursa za kujiajiri, kukabiliana na mazingira wanayoishia, kupata ujuzi zaidi wa elimu walizosomea pamoja na kupata mitaji itakayowawezesha kujiendeleza kimaisha”.

Aidha amesema kuwa ni muhimu pia kwa vijana kutumia vyema mitandao ya kijamii katika kutafuta fursa za kimaendeleo na kuacha tabia ya kutumia kwa matumizi yasiyofaa.

Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amewataka vijana kutoa ushauri sahihi kwa serikali juu ya njia bora na sahihi itakayosaidia vijana kutambua fursa na kuwa sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili katika mazingira wanayotoka.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.