Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel leo ameendelea kuongoza zoezi la kuwapatia mahitaji muhimu na ukaguzi wa ujenzi wa Bweni la Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bwiru lililoungua wiki hii.
Akiwa Shuleni hapo Mhe Gabriel amewakabidhi Wanafunzi 76 Masanduku, Nguo, Makufuli na Shuka za kulalia ambayo ni michango inayoendelea kutolewa na Wadau mbalimbali wa Mwanza walioguswa na janga la moto huo.
"Naomba mtulie msiwe na shaka na badala yake ongezeni bidii ya masomo, tambueni Serikali ipo nanyi ndiyo maana mnaniona tangu siku ya ajali ya moto nipo hapa kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa kama awali" Mkuu wa Mkoa.
Amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi wa Bweni na kuwataka Walimu wenye Taaluma ya Uhandisi kutoka Shule hiyo kushiriki ujenzi wa Bweni hilo na kuwahimiza wahusika wote kutanguliza uzalendo ili Wanafunzi hao wapate Bweni bora na la kisasa.
Katika hatua nyingine, Mhe Gabriel amefanya kikao kifupi na Walimu wa Sekondari ya Bwiru na kuwaahidi kuzitatua changamoto zao mbalimbali yakiwemo kuboresha nyumba zao za kuishi na mazingira ya kazi zao.
Baadhi ya Wanafunzi Michael Masatu na Shafii Said wakizungumza kwa niaba ya wenzao wamemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa msaada wa haraka walioutoa kwao mara baada ya Janga hilo la moto na kuahidi kusoma kwa bidii ili kutimiza malengo yao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bwiru Thomas Werema amewaondoa shaka wazazi wa Wanafunzi na kusisitiza mazingira yote yapo salama na Wanafunzi wanaendelea na masomo vizuri.
Bweni la Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bwiru liliteketea na moto siku ya Jumatano kuamkia Alhamisi na vitu vyote vilivyokuwemo kuangamia na moto huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.