Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi wa REA mkoani Mwanza kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati baada ya kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Akiongea kwenye kikao cha kwanza cha bodi ya barabara ya Mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Mhe.Mongella alisema REA limekuwa tatizo kwakuwa wananchi wa maeneo mengi hawajapata huduma licha ya REA awamu ya kwanza na ya pili kumalizika.
"REA kwa Mkoa wetu ni tatizo," alisema Mongella.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Magu Hilali Elisha akichangia katika kikao hicho alisema miradi ya REA haiendi vizuri wilayani Magu akibainisha ni vijiji viwili kati ya vijiji 27 ndivyo vimeanza kuunganishiwa umeme.
Akitoa ufafanuzi wa vijiji vilivyoonganishiwa umeme, Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoani Mwanza Mhandisi Lucas Mtabilwa alisema, Jumla ya vijiji 224 vimepata huduma ya umeme kupitia REA awamu ya kwanza na awamu pili na kufanya vijiji vyenye umeme kufikia 480 kati ya vijiji 758 vya Mkoa wa Mwanza ikiwa sawa na asilimia 63.3 ya vijiji vyote.
Mhandisi Mtabilwa alisema mradi wa REA awamu ya tatu unatarajia kugharimu Tshs. 22,999,376,085.42 na kuwa jumla ya vijiji 174 watanufaika na mradi huo.
"Awamu hii itahusisha ujenzi wa njia kubwa ya umeme yenye Urefu wa km 264.3, ujenzi wa njia ndogo yenye Urefu wa km 649, ufungaji wa transforma 319 na uunganishaji wa wateja wapya 10676," alisema Mhandisi Mtabilwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe.Juma Sweda aliwataka REA wajitathimini namna gani watafikia vijiji ambavyo vipo kwenye mpango kwa kuwa wananchi wanatarajia na wanahamu na umeme.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.