Serikali imezindua na kutangaza rasmi uwepo wa fursa za usafirishaji mizingo kupitia Ushoroba wa Kati (central corridor) katika Bandari ya Mwanza Kusini kwenda nchi za Uganda na Sudani Kusini.
Uzinduzi huo umefanyika eneo la Bandari ya Mwanza Kusini ambapo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe.Isack Kamwelwe amesema Serikali imefikia hatua ya kutangaza ushoroba wa kati kutokana na kuimarika kwa mifumo ya njia kuu za usafirishaji wa anga, ardhi, barabara, reli ,mabomba, maji, mifumo takwimu na waya.
Mhe.Kamwelwe amesema utafiti uliofanywa na Serikali umebaini ushoroba wa kati ni miongoni wa shoroba zenye zaidi ya njia kuu tatu za usafirishaji na kufafanua kwamba usafirishaji kwa njia ya reli na meli ni usafiri wa uhakika na wenye gharama nafuu zaidi hususan mizigo inayosafirishwa kwa masafa marefu.
“Kwa takwimu za Shirika la Chakula Duniani (WFP) zinaonyesha kuwa kwa kutumia njia hii ya usafiri huu unaokoa asilimia 40 ya fedha ikilinganishwa na gharama za kutumia njia mbadala.Usafiri wa reli na maji kupitia Ziwa Viktoria kwenda Portbell Uganda umeunganishwa katika mfumo ambao treni inapowasili katika bandari ya Mwanza huingia moja kwa moja kwenye meli ya mizigi bila kushuka makasha.
“Ni jambo la kujivunia kwani ni nchi chache katika Afrika zenye miundombinu iliyounganishwa kwa utaratibu huu, kuanzia sasa mzingo unaposhushwa katika bandari ya Dar es Salaam unapakiwa kwenye treni ya shirika la reli nchini (TRC) na kuja Mwanza, unapofika hapa mzigo haushushwi bali mabehewa yanaingizwa moja kwa moja kwenye meli ya mizigo,”alisema.
Kamwelwe ameongeza kuwa hivi sasa Serikali kupitia kampuni ya meli inamiliki meli moja ya mizigo inayoitwa MV Umoja yenye uwezo wa kubeba mabehewa 19 kwa wakati mmoja lakini kutokana na ongezeko la mahitaji na kwa kutambua umhimu wa kuwahudumia wananchi na nchi jirani, imekusudia kujenga meli kubwa yenye uwezo wa kubeba mabehewa 50 kwa wakati mmoja sawa na tani 3000.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania na Uganda tayari zimekubaliana kuweka utaratibu wa kuwa na kituo kimoja cha kufanya malipo kwa ajili ya mizigo ya kutoka Dar es Salaam, Mwanza hadi Portbell.
Amefafanua kuwa tangu utaratibu huo uanze kutumika Juni 24, mwaka huu jumla ya mabehewa 1165 sawa na tani 45750 zimesafirishwa kupitia ushoroba huo kwa njia ya reli na mali, kati ya mizigo hiyo mabehewa 874 sawa na tani 34,960 yalibeba mzigo wa WFP, hivyo shirika hilo la chakula limechangia asilimia 75 ya mizigo yote iliyosafirishwa kwa kipindi hicho.
Kwa upande wa Kiongozi wa WFP Tawi la Tanzania, Michael Dunford amesema uwepo wa shoroba ya kati umesaidia kupunguza gharama za kusafirisha vyakula kupitia Ziwa Viktoria ambapo kwa kuanzia Julai 2, hadi jana amesafiriksha mabehewa 18 kwenda Uganda kwa njia ya reli na maji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella ametoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na taasisi kwa ujumla kutoka Tanzania na nje ya nchi kutumia fursa ya uwepo wa shoroba ya kati kupunguza gharama ya usafirishaji na hivyo kuinua vipato vyao.
"Kuwepo kwa ushoruba huu kutachangia sana fursa ya uchumi kwa wana Mwanza na maeneo ya jirani watu wakiwa na uchumi unaoaminia na utulivu unakuwa mkubwa".alisema Mongella.
Pia alisema kuwepo kwa ushoroba wa kati ni fursa nyingine kwa mkoa wa Mwanza kukuza uchumi wa mkoa, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ambapo alisisitiza kwa uongozi wa mkoa utaendelea kuimarisha usalama wa watu na mali zao ili kila mmoja aweze kufanya shughuli zake kwa amani.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe.Mhandisi Robert Gabriel, Katibu Mkuu, Sekta ya Uchukuzi, Leonard Chamuriho na viongozi mbalimbali wa mashirika na taasisi za umma na binafsi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.