TIMU YA UFUATILIAJI MRADI WA HOSPITALI YA RUFAA UKEREWE YATINGA SITE
Tarehe 27 Desemba, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda alimkabidhi Site Mkandarasi M/S Dimetoclasa Real Hope Ltd kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali yenye hadhi ya rufaa kwa Tshs. Bilioni 25 katika hafla ya kusaini mkataba iliyofanyika kwenye kijiji cha Bulamba.
Leo tarehe 08 Februari, 2025 timu ya ufuatiliaji ujenzi wa hoapitali ya rufaa ya Mkoa imetinga site (Site meeting 2) kwa ajili ya kufuatilia ujenzi wa hospitali hiyo ili kujiridhisha na kasi ya ujenzi pamoja na utekelezaji wa makubaliano ya matakwa ya mkataba kwa masilahi ya wananchi wa kisiwani humo.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya miundombinu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mhandisi Chagu Ng'homa amesema mpango wa Serikali ni kuanza kutoa huduma za afya mara moja pindi tu mradi utapokamilika kwa sehemu hiyo ya kwanza na ndio maana ujenzi umejumuisha majengo muhimu.
Amesema, jengo la ghorofa lenye uwezo wa kubeba vitanda 180, jengo la kuhifadhia maiti, kazi za nje na jengo la umeme pamoja na ofisi za walinzi ni sehemu ya majengo ya awali kutekelezwa na kwamba ndani ya siku 545 (Miezi 18) yatakamilika na huduma zitaanza kutolewa mara moja.
Katika kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka, Mhandisi Chagu akiwa kwenye ukaguzi wa eneo la ujenzi amepiga simu ya moja kwa moja kwa Mhandisi wa Wakala ya Umeme vijijini (REA) na kumtaka afike kwenye eneo hilo ili kuona namna ya kupeleka mradi wa umeme kwa ajili ya utekelezaji wa mradi
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba amesema sambamba na ujenzi huo taratibu zingine za kupata vifaa vya tiba na samani zinaendelea ili kuhakikisha mara tu ujenzi ukikamilika huduma za afya zinaanza kutolewa kwa wananchi wa Ukerewe.
Kwa upande wa mkandarasi, Mhandisi John Bhoke amesema shughuli za kuweka uzio kwenye eneo hilo zimekamilika, uondoaji wa udongo wa juu pamoja na kuandaa vipimo na eneo la jengo kuu la mradi zimeshakamilika na kwamba kwa sasa kazi inatakayofuata ni ujenzi wenyewe.
Aidha, ametoa wito kwa Mkandarasi mshauri pamoja na msimamizi wa mradi kuendelea kushirikiana na kuwasiliana mara kwa mara ili kupata uelewa wa pamoja wa kufanikisha ujenzi huo kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha malipo hayachelewi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.