Ili Kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wanawake, wajawazito watoto wachanga na watoto chini ya mwaka mmoja kwa Mkoa wa Mwanza, vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya million mia moja vyakabidhiwa.
Haya yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella wakati wa zoezi la kukabidhi vifaa tiba hivyo kutoka mradi wa afya ya mama na mtoto (IMPACT PROJECT) wilayani Ukerewe.
Alisema lengo kuu la serikali ni kushirikiana na mradi huo ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga mkoani Mwanza.
"Leo nimekabidhi vifaa hivi vifaa tiba vilivyonunuliwa na mradi wa IMPACT, kwa ufadhili wa Serikali ya watu wa Canada (GAC) ambazo ni mashine za kutakasia vifaa 45, mashine za kupima wingi wa Damu 80, mashine za kupimia Pressure 80 + 80,Mashine za kupimia uzito za watu wazima105, mashine za kupimia uzito watoto wachanga 80, Seti za kuzalishia kwa njia ya kawaida 80 na drip standa vyote vitumike ipasavyo ili kutimiza malengo " alisema Mongella.
Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa alisema takwimu za afya ya uzazi Mkoa wa Mwanza (2017) zinaonyesha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga bado ni vingi ambapo kwa mwaka 2017 vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi vilikuwa 195 na asilimia 92 ya vifo hivyo vilitokea katika vituo vya kutolea huduma za afya, na vifo vya watoto wachanga katika umri wa mimba baada ya kuzaliwa vilikuwa 1452 na vifo vya chini ya mwaka mmoja vilikuwa 684.
Aliongeza kuwa vyanzo vya vifo hivyo kwa asilimia fulani vilitokana na uhaba wa vifaa tiba kwa ajili ya kusaidia huduma kwa Mama wajawazito na watoto wachanga.
Pamoja na jitihada hizo , Mkoa huo bado unakabiliwa na Changamoto kubwa ambazo ni pamoja na wanawake wajawazito kuchelewa kuanza kliniki, mila na Desturi potofu, mimba za mara kwa mara za mpishano mfupi kati ya mtoto na mtoto idadi kubwa ya akina mama kujifungulia nyumbani, elimu duni juu ya masuala ya afya changamoto katika mfumo wa rufaa haswa kwa maeneno yenye visiwa.
"Kweli uelewa duni wa dalili za hatari kwa mama mjamzito na mtoto Mchanga, ushiriki duni wa wanaume katika masuala ya afya ya uazi, uelewa duni juu ya lishe na ulaji unaofafaa kwa akina mama wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha na watoto kutonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 6 ya mwanzo, yote haya yanachangia hali duni ya afya ya Mama na mtoto na jamii kwa ujumla" alisema Rutachunzibwa.
Kwa upande wake Meneja mradi wa IMPACT Edna Selestine alisema kupitia utekelezaji wa mradi huo Shirika la Aga khan Development Network lina mikakati ya kupunguza vifo kwa kuboresha upatikanaji wa huduma na kuongeza matumizi ya huduma bora za afya kwa wanawake, wajaawazito, watoto wachanga na watoto chini ya mwaka mmoja.
Alisema ili kufanikisha malengo hayo, mradi huo umejikita katika Kutoa mafunzo maalum kwa watoa huduma za afya ili kuwajengea uwezo wa kutoa huduma stahiki kwa wakati muafaka, Kujenga majengo yanayolenga huduma za wajawazito na watoto wachanga katika vituo 24 vya kutolea huduma ndani ya Mkoa wa Mwanza na kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kutolea huduma na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
"Mradi huu utawezesha mafunzo mbalimbali ngazi ya jamii ikiwa ni pamoja na vipindi vya Redio , Televisheni, vikundi mbalimbali ili kufikisha jumbe zitakazowezesha mabadiliko ya tabia katika jamii ili mwisho wa mradi huu baadhi ya changamoto kama si zote zinazochangia vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga vitapungua au kuisha kabisa",alisema Selestine.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.