WADAU ZAO LA CHOROKO WAPEWA SOMO STAKABADHI GHALANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefungua mkutano wa wadau wa zao la Choroko wenye lengo la kuelimishana umuhimu wa matumizi ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
Akizungumza na wadau hao leo Januari 29, 2025 kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi ya mkuu wa mkoa, Mtanda amesema mkutano huo ni muhimu kwani mfumo huo utakuwa ni mkombozi kwa mkulima kwani ataweza kuuuza kwa bei nzuri na kuepukana na baadhi ya wajanja wachache wanaofaidika kwa ulaghai.
Mhe. Mtanda amebainisha huu ni mpango wa Serikali wenye nia njema ya kuhakikisha mkulima ananufaika na shughuli zake za shambani hivyo mazao ya jamii ya mikunde ambayo awali ilikuwa kama imesahaulika sasa iwe na tija kwao.
"Serikali imeunda Mamlaka ya udhibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko COPRA lengo ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa mazao hayo kuanzia kilimo bora kitakacholeta uvunaji bora pia na bei nzuri kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani",amesisitiza mkuu huyo wa mkoa.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya udhibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko COPRA, Irene Mlola amesema katika mfumo huo wataanza na mazao ya makundi matano ambayo ni nafaka ukiwemo mpunga na Mahindi,mbegu za mafuta ikijumuisha alizeti,michikichi, na ufuta,jamii ya bustani ni pamoja na maua na mbogamboga,jamii ya mikunde itajumuisha choroko,mbaazi,dengu na soya na jamii ya mizizi ni viazi,mihogo na magimbi
Aidha kaimu Katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Innocent Keya akizungumzia uzalishaji wa zao la Choroko mkoani Mwanza amebainisha kwa msimu wa mwaka 2023-24 Mkoa umevuna tani 16,862.
"Msimu huu wa Masika Mkoa wa Mwanza utakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani,wilaya za Kwimba,Magu,Misungwi na Sengerema zinazolima kwa wingi Choroko zitakuwa na mvua za milimita 350 hadi 400 ni vizuri wakulima wafahamu na kuzingatia taarifa hii ili wajipange vizuri,"Agustino Nduganda,mtaalamu kutoka Mamlaka ya hali ya hewani,TMA
Katika kikao hicho wadau wa mkutano huo ambao ni wenyeviti wa Halmashauri,wakuu wa wilaya wakulima, na wasambazaji wameitaka COPRA kuendelea kuufanyia utafiti mzuri mfumo wa Stakabadhi Ghalani kabla haujaanza kutumika rasmi mkoani Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.