Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Ameir (Mb) amesema wahitimu wa masomo ya Sayansi na Teknolojia wanahitajika kwa wingi zaidi nchini kwani Uchumi unategemea zaidi ujuzi wenye ubunifu, sayansi na teknolojia.

Ameyasema hayo leo Desemba 15, 2025 katika mahafali ya 19 duru ya pili ya chuo cha Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) kampasi ya Mwanza wakati akitunuku vyeti kwa wahitimu wa Astashahada na Stashada katika fani mbalimbali kwa niaba ya Waziri wa Wizara husika.

Aidha, Mhe. Wanu ameeleza kuwa katika kuongeza fursa kwa vijana serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeleta mradi wa DISTIC wenye thamani ya Billioni 37 chuoni hapo ili utakaofadhili mambo kadhaa ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kufundisha na kuchakata bidhaa.

Vilevile, amezitaja juhudi zingine za kuboresha ufundi stadi kuwa ni pamoja na uwepo wa Bilioni 15.27 zilizopatikana kupitia mradi wa TERMS II zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa vyuo vingine vya ufundi nchini.

Akiupongeza uongozi wa chuo hicho hasa kwa kushirikiana na mataifa kama Uingereza, Ureno na Ethiopia Mhe. Wanu ameeleza kuwa serikali imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wa taasisi za elimu ya ufundi stadi nchini kwa kutoa wakufunzi 912 wa mitaala inayoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Naye Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Said Mtanda amewasihi kupunguza kutoa mafunzo ya baadhi ya kada ili kujikita katika taaluma ambayo wahitimu watakapomaliza waweze kujiajiri na sio kujenga idadi kubwa ya wenye vyeti bila maarifa, ujuzi na ubunifu.

Halikadhalika, amewapongeza wahitimu na kuwataka na kuwasihi kujiunga kwenye vikundi na kuchukua mikopo serikalini isiyo na riba na kujenga vizimba vya kufugia samaki ili kumudu maisha kwani wamepata stadi za nadharia kwenye eneo hilo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.