WATUMISHI RS MWANZA WAFANYA ZIARA UTALII WA NDANI HIFADHI YA SERENGETI
Watumishi zaidi ya 30 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo Februari 14, 2025 wamefanya ziara ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SNP) kwa ajili ya kushuhudia vivutio mbalimbali vya utalii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa msafara huo Mkuu wa Seksheni ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi ndugu Kusirie Swai amesema ziara hiyo imelenga kutoa hamasa ya utalii wa ndani kwa watumishi wa Mkoa wa Mwanza.
Amesema sambamba na hilo ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutangaza na kukuza sekta ya utalii nchini kwa kutembelea vivutio mbalimbali.
Ndugu Swai amesisitiza kuwa ziara hiyo imewapa fursa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti ikiwemo wanyama wakubwa kama vile Simba, Tembo, Faru, Nyati na Chui wakiwa katika mazingira ya asili yaliyohifadhiwa vizuri.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Jesca Lebba akiwa ni miongoni mwa watumishi walioshiriki ziara hiyo ameushukuru uongozi wa Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Said Mtanda na Katibu Tawala Mkoa Bw. Balandya Elikana kwa juhudi kubwa wanazofanya kwa watumishi hao ambapo wameitaja ziara hiyo kuwa itakwenda kuongeza tija na hamasa katika utendaji wa majukumu yao kutokana na mapumziko mujarabu.
"Ziara hii ya kitalii itasaidia kuhamasisha watumishi wengi zaidi kutembelea hifadhi wakiwa na familia zao wakati mwingine kwa kuwa wameshaona umuhimu wa kufanya hivyo kiafya kwani inapunguza hata msongo wa mawazo”. Amesema ndugu Paulo Zahoro, Afisa Habari wa Mkoa.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni mbuga kubwa ya kitaifa ambayo ina urefu wa zaidi ya kilomita za mraba 14,763 Ipo mashariki mwa Mkoa wa Mara na kaskazini mashariki mwa Mkoa wa Simiyu na ina zaidi ya hekta milioni 1.5 Hifadhi hiyo ilianzishwa mnamo 1940.
Aidha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni urithi wa Dunia iliyojaa wanyamapori zaidi ya wanyama milioni 2, simba 4000, chui 1000, duma 550 na aina 500 za ndege wanaishi katika eneo linalokaribia kilomita za mraba 15,000 kwa ukubwa.
Watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wapo kwenye mpango thabiti wa kupumzika kwa kufanya utalii katika hifadhi mbalimbali nchini pamoja ni kuangalia utekelezaji wa miradi ya Kimkakati ambapo kesho februari 14, 2025 wanatarajia kutembelea Mamlaka ya Ngorongoro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.