WAZIRI BASHUNGWA AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUIMARISHA USAFIRI VISIWANI
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Fedha nyingi kukarabati na kujenga vivuko vipya katika kuimarisha Usafiri kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Visiwa kwenye Mikoa ya Kanda ya ziwa.
Ametoa pongezi hizo leo Oktoba 11, 2023 wakati wa ziara yake Mkoani Mwanza alipofika kwenye Karakana na Songoro Marine wilayani Ilemela kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Vivuko vipya Vitano vilivyogharimu zaidi ya Bilioni 20 na Ukarabati wa Vingine kikiwemo Kivuko cha MV Mara kilichogharimu zaidi ya Milioni 300.
Aidha, amewaagiza Kampuni ya Songoro Marine kuhakikisha wanakamilisha asilimia moja iliyobaki kwenye Ukarabati wa Kivuko cha MV Mara kwa mujibu wa Mkataba kufikia Oktoba 15, 2023 ili kikahudumie wananchi kwenye visiwa vya Wilaya ya Musoma ambao wanakosubiri.
"Nimefurahi kuona Songoro Marine mnajitangaza kwa kazi nzuri kimataifa, ongezeni nguvu mfanye kazi usiku na mchana ili kufikia Oktoba 15, 2023 mkamilishe ukarabati na niwatake TASAC kuja kukikagua kwa haraka ili kivuko hichi (MV MARA) kikawaondolee adha ya Usafiri wananchi wa Mara." Waziri Bashungwa.
Vilevile, Waziri Bashungwa ameagiza ukamilishaji wa Vivuko vya Rugezi- Kisorya (70%), Ijinga- Kihangara (67%), Bwiro- Bukondo (70%), Nyakalilo- Kome (55.5%), Butagu -Mbalika (30%), MV Nyerere na MV Kilombero ili vikawahudumie wananchi na kutimiza adhma ya Rais Samia ya kuboresha huduma za Usafiri wa Majini.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuboresha huduma za Usafiri kwa kuhakikisha wananchi wanapata vivuko ambavyo ni bora na salama viwapo majini na amempongeza Mkandarasi Mzawa Songoro Marine kwa utekelezaji wa miradi kwa uzalendo.
"Hapo zamani kwenye maeneo ya ziwa kulikua na ajali za mara kwa mara kutokana na kutumia Mitumbwi ambayo sio salama, Mhe. Rais amedhamia kufuta kabisa adha hizo na kwa upendo mkubwa tunaona amekua akileta mabilioni ya fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga vivuko katika maeneo mbalimbali". Amesema Mkuu wa Mkoa.
Katika wakati mwingine Waziri Bashungwa amehudhuria Mkutano wa Bodi ya Usajiri wa Makandarasi na amewataka wakandarasi wa ndani kuheshimu taaluma yao, kuwa wabunifu na kuhakikisha wanatekeleza miradi katika hali ya ubora ili kulinda fedha nyingi zinazotolewa na Serikali na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuaminiwa.
Akihitimisha ziara yake Mkoani Mwanza, Waziri Bashungwa amekagua ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa Kilomita 3.2 linalojengwa kwa zaidi ya Bilioni 700 na amemuagiza Mkuu wa Mkoa kumsimamia Mkandarasi anayejenga daraja hilo ili akamilishe kwa wakati kwani serikali inafanya malipo kila wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.