WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAENDELEA KUTOA ELIMU YA URAIA NA UTAWALA BORA MWANZA
Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutoa mafunzo ya sheria kwa watendaji wa Serikali ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na haki katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.
Wakili wa Serikali Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Dorice Dario akizungumza leo wilayani Sengerema katika mafunzo amesema lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kuwa watendaji wa Serikali wanapata uelewa mzuri wa sheria ili kutenda haki kwa wananchi pindi wanapo timiza majukumu yao.
Wakili Dario, amesisitiza kuwa kuelekea uchaguzi mkuu nchini ni muhimu kwa kila mtendaji kufuata misingi ya sheria na kuheshimu haki za raia.
“Tunataka kuona watendaji wa kata na maafisa usalama wanatekeleza majukumu yao kwa haki na usawa kupitia mafunzo haya tunaimarisha uelewa wao kuhusu sheria ili kuepusha ukiukwaji wa haki za binadamu,” amesema Wakili.
Naye, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Nuru Mwambuli amehimiza watendaji kuzingatia misingi ya 4R za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Kujenga Upya katika utendaji wao wa kila siku.
Amebainisha misingi hii ni muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka na wananchi wanapata huduma bora za kisheria.
“Uzalendo kwa Taifa letu unapaswa kuwa nguzo ya msingi kwa kila mtendaji wa Serikali. tunapaswa kuhudumia wananchi kwa haki, bila upendeleo, na kuhakikisha kuwa tunapiga vita ukatili wa aina zote,” Wakili Nuru.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.