Serikali imesisitiza umuhimu wa kudhibiti mianya inayoweza kutumika na baadhi ya asasi za kiraia (Non-Profit Organizations) kufadhili vitendo vya kigaidi, ikiwa ni sehemu ya mapambano ya kitaifa na kimataifa dhidi ya ufadhili wa ugaidi na fedha haramu.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndg. Daniel Machunda amesema kumekuwa na ongezeko la wasiwasi duniani juu ya uwezekano wa baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kutumiwa kufadhili ugaidi, hivyo ni wajibu wa wadau wote kushirikiana kuhakikisha udhibiti huo unafanyika mapema kabla haujawa tishio.
Ameeleza kuwa mapambano hayo yanapaswa kuwa endelevu huku Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiendelea kutekeleza sheria na kanuni za kudhibiti fedha haramu, ufadhili wa ugaidi pamoja na biashara ya silaha za maangamizi.
Aidha, Machunda amezitaka asasi za kiraia nchini kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli zao, ili kulinda taswira njema na kuondoa mashaka yoyote yanayoweza kujitokeza katika jamii au kwa wadau wa kimataifa.
Pia ametoa shukrani kwa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit – FIU) kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, Ofisi ya Kabidhi Wasii (RITA), Non - Profit Organizations ( NPOs), Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) pamoja na Shirika la Ufadhili la Ujerumani (GIZ) kwa kuhakikisha semina na elimu juu ya udhibiti wa vitendo hivyo zinaendelea kutolewa kwa wadau mbalimbali nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.