**ATCL yashauriwa kwenda na wakati ili wasafirishaji wa mizigo nje ya nchi wamudu soko la ushindani.*
Wasafirishaji wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi wameomba waendeshaji wa ndege ijayo ya mizigo kuzingatia muda wa kutoka nchini, ili waweze kumudu ushindani katika masoko ya dunia.
Wametoa wito huo leo Jijini Mwanza wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya wadau uliondaliwa na shirika la ndege nchini (ATCL) ulioangazia juu ya nini kifanyike ili ndege hiyo ilete tija kwao na kwa nchi.
Ndege ya Shirika la ATCL aina ya B767-300F inatarajia kuwasili nchini wiki ijayo na ina uwezo wa kubeba tani 54.
Mhakiki Ubora Kampuni ya Victoria Perch inayosindika minofu ya samaki, Edwin Okong’o amesema inapotokea ndege ikachelewa hata kwa saa moja tu, tayari mteja wake huko nchi za Ulaya anapata hasara.
“Lakini hata sisi tunapoteza nafasi ya kushindana kibiashara. mara zote mteja wetu anaendana na ratiba ya mnada wa siku husika huko kwao, hivyo anapaswa kupokea mzigo kwa wakati ili auze ukiwa na ubora wa asili (fresh). Amesisitiza Okongo
Ameongeza kuwa usafirishaji wa mizigo unahitaji umakini na nidhamu ya hali ya juu ya kuzingatia muda tofauti na hapo wasafirishaji kutoka Tanzania wataonekana wababaishaji kwenye soko la Dunia.
Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe.Adam Malima ameunga mkono hoja hiyo na wakati huohuo amewataka wafanyabiashara kuzingatia suala la ubora wa bidhaa zao ili kumudu ushindani katika masoko ya kimataifa.
Ametolea mfano wa bidhaa za mifugo hasa nyama kwamba wazalishaji wanapaswa kuzingatia umri wa ng’ombe kuchinjwa, ambao si zaidi ya miaka miwili na nusu.
“Lakini pia muungane ninyi na wafanyabiashara wengine wa mikoa ya kanda ya ziwa, ili kuwe na mzigo wa uhakika kujaza ndege hiyo"RC Malima
Mtendaji Mkuu ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, amebainisha utakuwepo uhakika wa bidhaa za Tanzania kufika sokoni kwa wakati kutokana na uwepo wa ndege ya serikali ya mizigo.
“Maana yake itakua ikiruka moja kwa moja kutoka nchini kwetu hadi mwisho wa safari ni tofauti na tulivyokua tukitegemea ndege za wenzetu nchi jirani".Amesema Mhanisi Matindi
Mbali na mazao ya uvuvi na mifugo, Matindi amesema ziko nchi nyingi zenye mahitaji ya mazao jamii ya kunde na maharage, lakini pia mbogamboga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.