BARABARA YA LAMI YANOGESHA UTALII KUELEKEA MAKUMBUSHO YA BUJORA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilayani Magu imejenga barabara ya kiwango cha lami nyepesi Kisesa -Bujora yenye kilomita 1.23 kwa zaidi ya Tshs. Bilioni 1.4 ambayo itachochea utalii kuelekea kituo cha Utamaduni cha Bujora na Makumbusho ya kabila la Wasukuma.
Amebainisha hayo leo Septemba18, 2024 wakati akikagua mradi huo muhimu kwenye eneo la Bujora ambapo amefafanua kuwa pamoja na kuchagiza utalii itasaidia pia kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao ya kilimo kwa wananchi wa Bujora, Kanyama na Kisesa Wilayani Magu.
Aidha, Mhe. Mtanda ametoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo na kuhakikisha inakua kwenye hali ya usafi wakati wote na akawaagiza TARURA kuweka taa za barabarani kwenye eneo lililobaki ili kuwahakikishia wananchi usalama wakati wanaitumia barabara hiyo.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA wilaya ya Magu Mhandisi Musa Mzimbili amefafanua kuwa mradi huo ambao umekamilika tangia 2023 umehusisha ujenzi wa barabara, mitaro ya maji, vivuko vya watembea kwa miguu, makaravati pamoja na taa 400.
Katika wakati mwingine, Mkuu wa Mkoa amekagua ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha Afya Nyanguge inayojengwa kwa zaidi ya Milioni 250 za mapato ya ndani ambapo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Magu kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.