BITEKO AWATAKA WAANDISHI WAENDESHA OFISI KUJIENDELEZA KITAALUMA
*Amewataka Waajiri kujali maslahi ya kada ya Waandishi Waendesha Ofisi*
*RC Mtanda amemshukuru Rais Samia kwa Utekelezaji wa miradi Mikubwa Mwanza*
*Abainisha pia utoshelevu wa Umeme kwa wananchi wa Mkoa huo*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Waandishi Waendesha Ofisi kujiendeleza kitaaluma ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia hususani kidigiti kwani ndiko kwenye muelekeo wa dunia ya sasa.
Amesema hayo leo 23 Mei, 2024 wakati akifungua rasmi Mkutano wa kumi na moja wa Kitaaluma wa Waendesha Ofisi unaofanyika kwa siku sita kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mkoani Mwanza chini ya Uratibu wa Chama cha Makatibu Mahsusi (TAPSEA).
Dkt. Biteko ametoa wito kwa waandishi waendesha ofisi hao kubadilisha utendaji kazi kwa kujali wananchi na kuhakikisha wanatatua changamoto zao kwa upendo na uamuzi bora wa utendaji kazi ili kuleta tija kwa Serikali yenye matarajio makubwa kwao.
Aidha, ameziagiza Wizara husika kuhakikisha wanakomesha kero na changamoto zinazowakabili waandishi waendesha ofisi hao kwa kuzingatia matakwa ya muundo mpya wa utendaji wa kada hiyo na kuhakikisha waajiri wanajali maslahi yao.
Mhe. George Simbachawene (MB), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora ametumia jukwaa hilo kuwataka kuwa mabalozi wazuri kwa waajiri wao kwa kuwa wabunifu na wenye utendaji kazi wa kuzingatia maadili zaidi na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha kada hiyo.
Hata hivyo, ameahidi kutoa waraka kwa taasisi zote kuboresha muundo wa waandishi waendesha ofisi kwa kuzingatia majukumu mapya yanayoenda sambamba na muundo mpya wa kada hiyo ulioanza mwezi Juni 2023 baada ya Mhe. Rais kuridhia maboresho ya kada hiyo ikiwa ni pamoja na ajira kuanza na ngazi ya stashahada.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaja miradi inayotekelezwa Mwanza kama wa Umeme Vijijini wa REA wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 56 kabla ya ile ya Ujazilizi inayogharimu zaidi ya Bilioni 12 na amebainisha kuwa Mwanza inatumia Megawati 76 pekee za umeme pamoja na kuwepo kwa Megawati 153.
Vilevile, ameitaja miradi ya upanuzi na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege, ujenzi wa Meli ya kisasa ya MV Mwanza, mradi wa maji Butimba, ujenzi wa vivuko vya kisasa na akabainisha kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha umahiri mkubwa kwenye kuongoza Taifa kwani miradi hiyo ipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji.
Mwenyekiti wa TAPSEA Bi. Zuhura Songambele amesema chama hicho kipo imara huhakikisha kinakuza uwajibikaji, kusaidia wanachama kuendeleza taaluma yao pamoja na kuwakumbusha kutoa huduma bora kwa viongozi na wananchi kwa weledi.
Mkutano huo wa kumi na moja uliowakutanisha zaidi ya wanachama elfu tano unaendeshwa kwa juma zima chini ya Kauli Mbiu isemayo ; Mafanikio huanza na uamuzi bora wa Utendaji, tutumie muda vizuri kwa kufanya kazi na kuleta Tija.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.