BODI YA BONDE ZIWA VICTORIA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA KISEKTA KUMALIZA MAGUGU-MAJI ZIWANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewaagiza Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria kushirikiana na Wadau wa Kisekta kuandaa na kuja na mpango mkakati wa kumaliza changamoto ya magugu-maji ndani ya ziwa Victoria.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo alipokutana na Taasisi zinazofanya shughuli za utunzaji wa mazingira, mabadiliko ya tabia nchi na mashirika yanayoshugulika na mazingira ambapo amewataka kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika suala zima la utunzaji wa mazingira mkoani Mwanza.
Aidha, Mhe. Mtanda ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamekuwa yakijulikana kwa shughuli za utunzaji mazingira kuhakikisha wanakuwa na matokeo chanya na siyo kuishia kuwa mashirika ya mfukoni.
“Nina mkeka mrefu sana wa NGO’s na taarifa za fedha wanazopokea kutoka sehemu mbalimbali za kutunza mazingira lakini wengi wenu mmekuwa hamfanyi hivyo”. Amesisitiza Mhe. Mtanda.
Sambamba na hilo, ameyataka mashirika hayo kuwasilisha shughuli wanazokuwa wanafanya kwa maana bila ya kufanya hivyo wataonekana hawafanyi kazi, Kadhalika amewataka uwepo wa tathmini za shughuli zote za mashirika namna walivyoshiriki katika utunzaji wa mazingira.
Kabla ya kufunga kikao chake, Mhe. Mtanda ameahidi kuwaleta Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pamoja na Wizara ya Maji kuja kukaa na wadau kupanga mipango ya kutunza mazingira katika Mkoa wa Mwanza.
Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza Bi. Janeth Shishila amesema kwa Mkoa wa Mwanza kuna mashirika 650 yaliyosajiliwa kufanya kazi zake na kuyataka yanahusika na mazingira kuhakikisha wanafanya kazi zao ipaswavyo kwa kuwa fedha wanazo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.