Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kujenga utumishi wa umma ulio imara, wenye motisha, unaozingatia maadili na unaoleta tija kwa wananchi kupitia programu mbalimbali ikiwemo michezo kwa watumishi wa umma.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda wakati akifungua Bonanza la Michezo kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka lililofanyika katika Viwanja vya CCM Kirumba, Jijini Mwanza, tarehe 20 Desemba, 2025.

Mhe. Mtanda amesema bonanza hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali inayolenga kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na afya njema ya mwili na akili, mshikamano kazini na uadilifu wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameeleza kuwa majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yanahitaji umakini mkubwa, uzingatiaji wa sheria, ujasiri wa kufanya maamuzi magumu na msimamo thabiti wa kimaadili. Hivyo, mazingira ya kazi yenye mshikamano na ushirikiano huchangia kwa kiasi kikubwa ufanisi wa taasisi.

Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa michezo na burudani ni nyenzo muhimu ya kuondoa msongo wa mawazo, kuimarisha afya na kujenga moyo wa kufanya kazi kama timu moja.

Aidha, amesema Serikali inatarajia matukio kama haya yaendelee kutumika kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wa haki jinai, jambo litakalosaidia mapambano dhidi ya uhalifu na rushwa.

Kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mtanda ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylivester Mwakitalu amesema bonanza hilo limeandaliwa kwa lengo la kuimarisha afya za watumishi pamoja na kuongeza ufanisi na ari katika utendaji kazi wa kila siku.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.