CCM MWANZA YAKAGUA MIRADI YA ZAIDI YA SHS BILIONI 20 SENGEREMA,YAMSHUKURU RAIS SAMIA, YAMPONGEZA RC
Kamati ya Siasa Mkoani Mwanza leo imeanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na ikiwa wilayani Sengerema imekagua miradi 5 yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 20 na kumshukuru Rais Samia kwa kuzidi kusukuma mbele maendeleo ya wananchi na kumpongeza pia Mkuu wa Mkoa Mhe.Said Mtanda kwa usimamizi mzuri.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Michael Lushinge akiambatana na Mkuu wa Mkoa Mhe. Said Mtanda imekagua mradi wa maji uliopo Nyasigu-Lubungo-Ngoma unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Sengerema (SEUWASA) uliogharimu zaidi ya shs bilioni 13, Kamati hiyo imefurahishwa na maendeleo yake licha ya kucheleweshewa malipo yake ya zaidi ya shs bilioni 2 na kuitaka Serikali kuhakikisha analipwa kwa wakati ili awahi kumaliza mradi huo.
"Hii ni hatua nzuri nimesikia mradi huu wenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 12 kwa siku ukikamilika utawanufaisha wananchi wapatao 52,800 kutoka kata za Igalula na Kagunga,Mhe.Mkuu wa Mkoa hakikisha fedha hizi zinapatikana ili wananchi wapate huduma hii muhimu", Mhe. Lushinge.
Amesema Rais Samia ana kila sababu kumshukuru kutokana na kuleta fedha nyingi za miradi mkoani Mwanza,na wajibu wa Serikali ni kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuwa na tija kwa wananchi.
"Mhe.Mwenyekiti mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa hapa wilayani kwetu, mwanzoni ulianza kwa kusuasua ulivyokuwa unasimamiwa na MWAUWASA kabla ya kukabidhiwa SEUWASA na sasa umekuwa na kasi nzuri,"Senyi Ngaga,Mkuu wa Wilaya Sengerema.
"Kazi inayokwenda kufanyika sasa ni utandazaji wa mabomba ya maji kwenye maeneo yote husika ili wananchi waanze kupata huduma hii mwishoni mwa mwaka huu",Saadi Hamisi,Meneja SEUWASA
Kamati hiyo ikiwa Sengerema mjini imekagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri hiyo unaotekelezwa na mkandarasi Suma Jkt kwa gharama ya zaidi ya shs bilioni 3,lakini taarifa imesema bado mkandarasi anadai malipo ya zaidi ya shs milioni 300 ili kuendelea na ujenzi,na Mwenyekiti wa CCM kuagiza Serikali kuharakisha malipo hayo ili huduma kwa wananchi ziendelee.
Kamati hiyo ikiwa inamalizia ukaguzi wa miradi hiyo imetembelea ujenzi wa jengo jipya la Mamlaka ya Mapato Sengerema,TRA lenye gharama ya zaidi ya shs bilioni 2 lililofikia asilimia 85 kukamilika.
"Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kupitia Wizara ya Fedha kwa kutupatia fedha kujenga jengo hili ambalo litaturahisishia shughuli zetu za ukusanyaji mapato na kazi kuwa na tija zaidi,"Henry Raymond,Meneja TRA Sengerema.
Ikihitimisha ziara hiyo ya ukaguzi kwenye ujenzi wa uwanja wa michezo eneo la mnadani uliogharimu zaidi ya shs milioni 300,Mkuu wa Mkoa Mhe.Said Mtanda amewahakikishia wakazi wa Sengerema utawanufaisha kimapato kwani timu ya Pamba Jiji FC itakuwa inakuja kupiga Kambi hapo na siku ya ufunguzi atawaletea msanii mkubwa hapa nchini.
Katika kikao kifupi cha tathmini Mhe.Mtanda ameishukuru kamati hiyo kwa uamuzi wa kufanya ziara hiyo ambayo imeisaidia Serikali kuona mapungufu yaliyobainika na kuahidi kuyafanyia kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.