CHIFU HANGAYA AZINDUA RASMI TAMASHA LA BULABO MWANZA, ATAHADHARISHA UUZAJI HOHELA WA CHAKULA
*Amewataka watanzania kutunza Chakula wanachovuna*
*Amekipongeza Kituo cha Utamaduni cha Bujora kwa kutunza Utamaduni*
*Aagiza Mikoa kujenga Maghala ya Chakula*
*Aagiza Machifu kulea vijana kimadili na kutunza mazingira*
*Aagiza Utamaduni kufungamanishwa na Utalii*
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Juni 13, 2023 amezindua rasmi Tamasha la Utamaduni wa ngoma za asili nchini ambalo katika tamasha la miaka miwili iliyopita alikabidhiwa Uongozi wa Machifu na kuitwa Chifu Hangaya.
Akizungumza na maelfu ya wananchi kwenye viwanja vya Msalaba Mwekundu- Kisesa Mkoani Mwanza, Chifu Hangaya ametoa tahadhari kwa watanzania kutouza chakula wanachovuna kiholela hususani nje ya nchi badala yake amewataka kukitunza kwa ajili ya chakula cha familia ili kukabililiana na mfumuko wa bei.
"Nitoe wito kwa wakulima kutunza chakula cha kutosha kwani nchi yetu sasa tunataka iwe na akiba ya Chakula hadi tani laki 5 na Wizara itavinunua ili tuweke kwenye akiba yetu nchini na niwaombe wananchi tusiuze chakula chetu nje ya nchi na wizara ya Kilimo na Fedha nimeshawaagiza kutekeleza hili mara moja." amesema Mhe. Rais.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeanza usajili wa wakulima ili kujua ni watanzania wangapi wanalima na kwa kiwango gani na la pili itaendelea kutoa Mbolea ya ruzuku pamoja na kujenga Skimu nyingi zaidi za umwagiliaji ili watanzania walime na kuvuna zaidi pamoja na kujenga Maghala ya kutosha na kwamba kila Mkoa utajenga.
"Ulimwengu mzima sasa unatarajia kuwa na upungufu wa chakula na hali hii ikitokea tutarajie kutakua na mfumuko wa bei kwenye chakula na hayo yanatokana na Ugonjwa wa Uviko, vikwazo kutokana na vita pamoja na mabadiliko ya tabia nchi hivyo Serikali tumeongeza bajeti kwenye masuala ya kilimo ili kukabiliana." Chifu Hangaya.
Vilevile, Mhe. Rais ametoa wito kwa Machifu nchini kusaidia kulea vijana kimaadili na kuhakikisha jamii inatunza Mazingira kwa ajili ya ustawi wa nchi kwa sasa na siku za baadae huku akitolea mfano kuwa endapo jamii itakata miti basi mvua itapungua nchini na kukaribisha upungufu wa chakula.
Akitoa Salamu za Wizara, Balozi Dkt. Pindi Chana Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ametoa wito kwa wananchi wa Mwanza na Mikoa ya Kanda ya Ziwa kuenzi Utamaduni, Mila na desturi kupitia Tamasha hilo linalowakutanisha kila mwaka na kwamba wanapaswa kuhamasishana kuwa wazalendo kwa Taifa lao.
Aidha, ametambulisha mfuko wa Utamaduni ambao unakusudia kuwanufaisha wasanii nchini kupitia Benki zilizopo kwenye maeneo yao na ametoa wito kwa vikundi vya sanaa nchini kujisajili kwenye mfumo maalum uliopo kwenye Halmashauri zao ili watambulike rasmi na kuweza kunufaika na mafunzo mbalimbali.
Akitoa Salamu kwa niaba ya wananchi wa Mwanza, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Amos Makalla amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali huku akiitaja kama zaidi ya Bilioni 1 zinazojenga Barabara kwa kiwango cha lami kuelekea kwenye makumbusho ya Bujora pamoja na zaidi ya bilioni 4 zinazojenga jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Magu.
Aidha, ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais kwa kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 94 kujenga Madarasa zaidi ya elfu mbili Mkoani humo na akajinasibu kwa upendo walioupata wana Mwanza kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama Daraja la Kigongo- Busisi, Meli ya MV Mwanza pamoja na Reli ya kisasa (SGR) na akabainisha kuwa uboreshaji wa Bandari ya Dar Es Salaam utaisaidia Mwanza kwa kupokea Mizigo.
"Mhe. Rais ninakuahidi nitashirikiana na wenzangu kutimiza matarajio uliyonayo kwangu ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sitakuangusha kwani umenipa wasaidizi wazuri na wachapakazi sana na hata jambo la Kageye (Ardhi) nitalifanyia kazi vizuri kwa maslahi ya Kanisa letu na Serikali."
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Mhashamu Askofu Renatus Nkwande amesema pamoja na Wamisionari kutoka Ulaya na Mataifa mengine kuingia Afrika kwa dhumuni la kueneza dini, Kanisa Katoriki linaendelea kulinda na kuhifadhi Mila na Tamaduni za waafrika pasipo kuzibadilisha na Tamasha la Bulabo ni matunda yake.
"Mtemi maana yake ni Kukata, Watemi walikata Misitu ili wapate sehemu ya kuishi na kutawala pamoja na kupata eneo la kulima mashamba lakini leo tumeona Baraka za Mungu kwa kufika kwako katika eneo hili na tumepata Mvua." amesema Askofu Nkwande.
Naye, Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni na Makumbusho Bujora, Padri Ananias Fikiri amesema kituo hicho kilichoanza Miaka ya 1950 kinaendelea kutunza mila za kisukuma kwa njia za nyimbo na vyakula, kuendeleza sanaa kama ufinyanzi, kutunza na kuendeleza mila kwa njia za mafunzo na kushauri waganga kutibu kwa kutumia miti ya asili na kutangaza utalii.
"Sherehe hizi zinaadhimishwa kwa kuomba Baraka kwa Mwenyezi Mungu na ni sherehe zinazounganisha mambo mawili yaani kufurahia tamasha la maua yaani Bulabo ambayo ni kusherehekea mavuno ya mazao shambani kwa kisukuma na Sherehe za Ekaristi za Kanisa Katoriki". Padri Fikiri
Katika nyakati tofauti Bi. Anthonia Sangalali, Mwenyekiti wa Machifu pamoja na
Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Machifu nchini, Chifu Aaron Nyamironda wametumia tamasha hilo kumshukuru Chifu Hangaya, Machifu wote na wananchi kwa kushiriki kwenye sherehe za uzinduzi wa Tamasha hilo ambao linatarajiwa kuhitimishwa mnamo Juni 17, 2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.