CUHAS BINGWA WA TAMSA CUP 2024/25, RMO MWANZA AWAPA KIKOMBE NA FEDHA TASLIMU
Katibu Tawala Msaidizi Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa amefunga rasmi michuano ya jumuiya ya wanafunzi wa udaktari kutoka chuo cha Bugando (CUHAS) na Mwanza University katika uwanja wa CCM Kirumba.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mtanange mkali wa fainali uliowapa ushindi timu ya Bugando waliowapa kichapo cha mabao saba kwa nunge vijana wa Mwanza University Dkt. Lebba amewapongeza washindi hao na amewakabidhi Kikombe pamoja na fedha taslimu kiasi cha Tshs. 750,000
Dkt. Lebba ametumia wasaa huo kuwapongeza wanafunzi hao kwa kuandaa michuano hiyo huku akibainisha kuwa michezo kama sehemu ya mazoezi inasaidia kuimarisha afya na kuondoa msongo wa mawazo na kuwafanya wawe timamu kiakili katika masomo darasani.
"Michezo ni sehemu ya mazoezi hivyo nawapongeza sana nyie binafsi kama Serikali ya wanafunzi kwa kuandaa michuano hii kwani itawaimarisha kiafya na kuwafanya muwe na utayari wa kupokea maarifa darasani." Dkt. Lebba.
Aidha, Mganga Mkuu amewapongeza wanafunzi hao kwa ubunifu hadi kufanikisha Kongamano la Kisayansi pamoja na kambi ya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza matukio waliyoyafanya mwishoni mwa mwaka 2024 na kuleta tija kwa jamii na Taifa.
Michuano ya TAMSA CUP 2025 imefanyika katika Viwanja vya CCM Kirumba Wilayani Ilemela kwa kipindi cha mwezi mmoja huku ikizikutanisha timu sita kutoka kwenye vyuo hivyo viwili vya Afya na Sayansi chini ya kaulimbiu isemayo “Michezo kwa Afya Bora ya Akili”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.