DKT. BITEKO ATAKA MIUNDOMBINU YA HOSPITALI YA MISHENI SENGEREMA KUTUNZWA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka watumishi wa Hospitali ya Misheni Sengerema na wananchi wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanatunza na kulinda vifaa na miundombinu ya jengo la kutolea huduma za upasuaji lililogharimu shilingi bilioni 5.4.
Mhe. Biteko amesema wafadhili waliofadhili mradi wa jengo hilo pamoja na vifaa vyake wanamatumaini makubwa kuwa miundombinu hiyo na vifaa vitatunzwa vizuri ili viweze kutumika kwa muda mrefu.
Naibu Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Novemba mosi 2024 wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jengo la upasuaji na mradi wa umeme wa jua (Solar) katika hospitali ya Misheni wilayani Sengerema.
Aidha, Mhe. Dkt. Biteko amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia inathamini sana mchango wa kanisa katika kuboresha huduma za kijamii kama vile Elimu, Afya, na huduma zingine hivyo kuahidi kuendelea kushirikiana katika kuboresha maisha ya wananchi.
Kadhalima Mhe. Naibu Waziri Mkuu ameendelea kuwataka Viongozi wa dini kote nchini kuendelea kuihubiri amani ya nchi yetu ambayo ndio tunu yetu hasa katika kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhakikisha Watanzania wanabaki kuwa kitu kimoja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema kwa upande wa Sekta ya Afya wao kama Serikali wanajivunia Hospitali, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Hospitali Kongwe ya Misheni ya Wilaya ya Sengerema iliyoanzishwa mwaka 1959 (yenye miaka 65) na vituo vingi vya afya ambavyo kwa hakika vimekuwa msaada mkubwa sana kwa taifa letu
Sambamba na hilo RC Mtanda amelihakikishia Kanisa Katoliki kwamba Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutimiza malengo yake ya kulijenga Kanisa na kuwahudumia watanzania.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la upasuaji lenye vyumba vinne linaloendeshwa na Shirika la Simba Health Foundation na msaada wa ukarimu kutoka Pharus Foundation ya uholanzi na Wadau wengine, Dkt.Marie Voeten, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo amesema jengo hilo lilianza kujengwa mwaka 2023 na kukamilika mapema Julai 2024 na tayari limeanza kutoa huduma.
Akitoa neno la shukrani Mhashamu Baba Askofu Flavian Matindi Kassala, Askofu wa Jimbo la Geita, amewashukuru wafadhili hao kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika na kukubali pia kutenga mfuko maalumu wa msaada wa matibabu kwa wananchi wanaoshindwa kukidhi gharama za matibabu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.