DKT. BITEKO ATOA WITO KWA WAHITIMU CHUO CHA SAUT KUWA WAZALENDO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe, Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania kwenda Kusaidia jamii kwa kutumia taaluma zao na kujiepusha na Rushwa ili kusaidia watanzania wasiojiweza na kuwainua kutoka kutoka sehemu walipo.
Dkt. Biteko ametoa wito huo leo tarehe 16 Disemba, 2023 wakati wa Mahafali ya Ishirini na Sita ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania yaliyofanyika kwenye Uwanja vya Raila Odinga chuoni hapo ambapo kwa nafasi ya Ugeni Rasmi wanafunzi 3066 wamehitimu katika ngazi mbalimbali.
Mhe. Biteko amesema anatamani kuona taaluma zao wanazitumia kwa manufaa ya kusaidia wenye uhitaji kwenye jamii kwa kutoa ujuzi na ubunifu kwa upendo na kwamba ili kutimiza hilo ni lazima wawe na hofu ya Mungu na wenye kutenda zaidi na sio kulalamika na kujihusisha na matendo ya Rushwa.
"Kusoma kwenu hakutathibitishwa kwa cheti mlicho nacho Mkononi bali kwa athari ya matendo yenu baada ya kuhitimu kule muendako, namna ya kukabiliana na matatizo au jinsi ya kusaidia jamii kupitia taaluma zenu na kwakua kule muendako kuna mapambano basi wenye nguvu watasimama na walio dhaifu wataachwa njiani." Dkt. Biteko.
Akijibu hotuba ya Makamu Mkuu wa chuo hicho, Mhe. Biteko ameahidi kuwa Serikali itarekebisha Barabara za Mitaa ambazo zina makorongo na amebainisha kuwa siku za usoni chuoni hapo zitawekwa taa kwa ajili ya kuweka mazingira salama ya wanafunzi hasa usiku na kwamba Mkandarasi wa Ujenzi huo ameshapatikana.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha SAUT, Askofu wa Jimbo Katoriki la Geita na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoriki Tanzania, Askofu Flavian Kasala amesema Baraza la Chuo hicho linamshukuru Rais Samia kwa Ulezi wa Vyuo nchini kupitia TCU na Bodi ya Mikopo na anaamini kuwa Viwango vya Udahili na Mikopo kwa wanafunzi itaongezeka ili kuendelea kuboresha Elimu Nchini.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwasihi wahitimu kuenenda kimaadili huko waendako kwa mujibu wa walivyolelewa na kwenda kukitangaza Chuo hicho kwa kuwa weledi na wenye ujuzi na ubunifu mkubwa katika kazi na kwamba kwa ambao hawataajiriwa waende wakatunie ujuzi walioupata kufanya kwa vitendo kile walichojifunza.
Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu, Makamu Mkuu wa Chuo hicho amebainisha kuwa kwenye Mahafali hayo wamehitimu jumla ya wanafunzi 3066 katika fani mbalimbali katika ngazi za Astashahada hadi Shahada ya Udaktari wa Falsafa ambapo 49% ni wanawake na 51% Wanaume na kwamba Maadili na Taaluma ndio nguzo ya Chuo hicho kwenye kutoa Elimu bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.