Elimisheni Wananchi kuhusu Athari za Mvua za El Nino na sisi watumishi wa umma tuwe mfano: Katibu Mkuu Yonazi
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jim Yonazi leo Januari 20, 2024 ametembelea maeneo yaliyo athirika na mvua za el nino Mkoani Mwanza na kutaka wananchi wapate elimu ya kutosha kutokana na mvua hizo ikiwemo ujenzi bora wa nyumba zao.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Serikali akiambatana na mwenyeji wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amesema baadhi ya madaraja aliyopita kuona yalivyoharibiwa na mvua yamepakana na makazi ya watu hali ambayo ni hatari kwa usalama wao.
"Nimeanzia kuona hili Daraja la Mwananchi, Sinai, Mabatini na Mto Mirongo hali si Shwari kwa wakazi jirani na maeneo haya niwaombe sana watumishi wenzangu tuanze kuwa mfano wa jambo hili na tusiwe sehemu ya matatizo", amesisitiza Katibu mkuu huyo.
Amebainisha bado mvua zipo kwa mujibu wa mamlaka za hali ya hewa,hivyo ni wajibu kwa viongozi kuweka mkazo wa elimu ili kuepuka maafa na Serikali kuingia gharama kama ilivyotokea huko Hanang Mkoani Manyara.
"Ndugu Katibu mkuu hali hii unayoiona imechangiwa sana na ujenzi holela wa makazi ya wananchi na kusababisha njia za asili za kupita maji kukosekana hivyo maji kuchepuka sehemu zenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu",Balandya
Kwa upande wake Meneja wa Tarura Mkoa wa Mwanza Mhandisi Makori Kisare amesema zimetengwa jumla ya sh bilioni 11 ili kufanya marekebisho yote ya barabara na wameanza kufanya ukarabati mkubwa Daraja la Mwananchi.
Awali akitoa taarifa fupi ya Mkoa wa Mwanza hasa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu Mtendaji huyo wa Mkoa amesema Mwanza imepata jumla ya maambukizi 112,wagonjwa 92 wametibiwa na kuruhusiwa,19 wapo kwenye vituo vya afya na maambukizi mapya ni 12,wagonjwa 10 kutoka Nyamagana,Ilemela 1 na Ukerewe 1.
Katibu mkuu huyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amefanya ziara fupi ya siku moja Mkoani Mwanza kwa lengo la kuona athari za mvua hizo na kutoa maelekezo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.