ENDELEZENI WAJIBU WA KAZI NA MTENDE HAKI: MWENYEKITI TUGHE TAIFA
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyajazi Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa Bw. Joel Kaminyonge leo Mei 8, 2024 amezungumza na Wafanyajazi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kusisitiza uwajibikaji mahali pa kazi na kutenda haki.
Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa kila mfanyakazi ana wajibu wa kutimiza majukumu yake ipasavyo ambayo yataleta tija kwa maslahi yake na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
"Tunapotimiza majukumu yetu ni lazima pia haki zetu Wafanyajazi zizingatiwe kutoka kwa mwajiri, migogoro tunayoisikia mara nyingi chanzo kinaanzia hapo," Kaminyonge.
Katika mazungumzo hayo Mwenyekiti huyo amefafanua suala la kikokotoo ambalo limekuwa mwiba mkali kwa Wafanyajazi wanaostaafu na kusema Rais Samia ametoa muda wa mazungumzo kwa lengo la kufikia mwafaka mzuri baina ya Serikali na Shirikisho la Wafanyajazi TUCTA.
Aidha ametoa pongezi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kutokuwa na mashauri ya kinidhamu hali inayoonesha Wafanyajazi wanatimiza vizuri wajibu wao na uhusiano mzuri uliopo baina ya RS na tawi la TUGHE.
Akitoa taarifa fupi kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa kabla ya mgeni rasmi kuzungumza na wafanyajazi,Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Bw.Daniel Machunda amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ipo katika mahusiano mazuri na wafanyajazi wake
,na kukuomba uongozi wa TUGHE Taifa kuona namna ya kupunguza ada za ushiriki wa vikao mbalimbali vya kisekta kwa watumishi.
"Ndugu Mwenyekiti ada za ushiriki ni kubwa inafika hadi laki nne kwa mtu mmoja sasa hii inachangia kumgharamia mtu mmoja wanapohitajika zaidi ya mmoja,"amesisitiza Machunda.
Katika mkutano huo pia wanachama wapya 7 wa tawi la TUGHE Ofisi ya Mkuu wa Mkoa walithibitishwa na kupewa udhamini na Mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo akiwa Mkoani Mwanza atafanya ziara na kuzungumza na wafanyajazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Seko Toure na Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Bugando na Manispaa ya Ilemela.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.