FAMILIA ZIIMARISHWE ILI KULINDA KIZAZI CHA WATOTO:RAS BALANDYA
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Bw.Daniel Machunda ametaka kuwepo na mipango endelevu ya elimu kwa familia ili ziimarishwe na kuwa Taasisi imara za malezi ya watoto na hatimaye kuwa na Taifa lililo staarabika.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa kwenye kikao kazi cha kutathmini malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kuanzia miaka 0-8 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Tanroad,Machunda amebainisha msingi imara wa malezi ya mtoto unaanzia ngazi ya familia na endapo eneo hilo kukiwa na ulegevu tabia ya mtoto inaanza kuharibikia hapo.
"Ndugu zangu washiriki wa kikao kazi hiki nawaombeni sana mkalifanyie kazi jambo hili,Dunia sasa imekumbwa na changamoto nyingi hasa mabadiliko ya teknolojia,vitendo vya ukatili pia na umasikini,mkazo wa elimu kwa familia ni lazima uzingatiwe",Machunda
Amesema bado familia nyingi haziwajibiki ipasavyo katika malezi ya watoto wao na badala yake wanatumia muda mwingi katika shughuli zao za kuzipatia kipato familia na kufanya mtoto kupitia hatua mbalimbali hatarishi.
Amewataka washiriki hao ambao ni Maafisa Lishe,Ustawi wa Jamii,Maendeleo ya Jamii na Mipango kuhakikisha wanakuwa wabunifu wazuri katika kuielimisha Jamii kuhusu umuhimu wa malezi ya mtoto.
"Mtoto anatakiwa kulelewa katika misingi mikuu kama kumjua Mungu kwa Imani yake ya dini,kuheshimu watu wakubwa,kupata elimu na kupata nahitaji ya msingi kama chakula,afya,ulinzi na malazi",amefafanua Machunda wakati akitoa mada kwenye kikao kazi hicho.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia dawati la mtoto Bi.Merry Shilla amesema kwa kutambua umuhimu wa malezi ya mtoto wamejipanga kuwajengea uwezo Maafisa wake wa ngazi zoto mikoani ili kuwepo na muendelezo mzuri wa malezi ya mtoto.
"Bado kumekuwa na vitendo vya ukatili kwa watoto na pia kukosa malezi imara kutoka kwa familia, hizi changamoto hatuna budi kukusanya nguvu kwa pamoja ili kukabiliana nazo",Shilla
Kikao kazi hicho kimewashirikisha Maafisa Ustawi wa Jamii,Maendeleo ya Jamii,Maafisa Lishe,Mipango na Waganga wakuu wa Wilaya kutoka Halmashauri zote 8 za Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.