Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imepokea wageni kutoka Korea ya Kusini wakiwakilisha Kampuni za uwekezaji zilizopo Nchini humo kwa ajili ya kutafuta fursa za uwekezaji Mkoani Mwanza baada ya kutembelea Tovuti ya Mkoa na kusoma Mwongozo wa Uwekezaji.
Akiwatambulisha wageni hao, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Wazawa yenye makazi yake Zanzibar ijulikanayo kama Drums of Africa Limited Bwana Harun B. Mohamed ambaye ni mwenyeji wao amesema, Kampuni yake imepokea wageni hao wakiwa ni Kampuni mbili tofauti (U & I International) na (EK Engineering) na wana nia na uwezo wa kutaka kuwekeza Mkoani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewakaribisha wawekezaji hao na kuwaambia kuwa Mkoa umejipanga kuhakikisha kwamba unafanikisha sera ya viwanda na kuifanya Tanzania kuwa ni Nchi ya uchumi wa kati kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
“Kwa kuwa mmeonyesha nia ya kuwekeza Mwanza sisi tumefarijika na tupo tayari kuwapa ushirikiano wa hali ya juu kulingana na maeneo mtakayotaka kuwekeza” alisema Mongella.
Aidha, Mhe. Mongella amewataka wawekezaji wote wa ndani na nje kufika Mwanza kuona fursa na kuwekeza kwa kuwa uwekezaji Mwanza unatija kubwa kwa mwekezaji kwani Mkoa umejipanga, pia ni sehemu inayofikia kwa urahisi zaidi.
Naye, Bwana John Kim akiwakilisha Kampuni ya U & I International amesema amefarijika sana na mapokezi kwani ni mara ya kwanza kufika Mkoani hapa, hivyo wanakwenda kupitia mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mwanza waone ni sehemu gani wanaweza kuwekeza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.