FURSA ZA UWEKEZAJI MWANZA ZIPO ZA KUTOSHA KUANZIA VIWANDA, MADINI, UVUVI NA UTALII: RAS MWANZA
Timu ya wafanyakazi kutoka Ofisi ya Gavana Jimbo la Jiangsu nchini China leo Agosti 15, 2024 imefanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza aliyewakilishwa na Bw. Daniel Machunda ambaye ni Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano na jiji la Mwanza katika nyanja mbalimbali.
Akizungumza na wafanyajazi hao Machunda amesema uhusiano huo utakuwa na tija kwa pande hizo hasa kutokana na Mkoa wa Mwanza kuzidi kuimarika kiuchumi na kuwepo eneo la kimkakati huku China ikizidi kupaa kwa teknolojia Duniani.
Aidha, Machunda amebainisha kuwa Gavana wa Jimbo hilo Mhe. Xu Kunlin anayetarajiwa kuja mwishoni mwa mwaka huu atavutiwa na fursa nyingi atakazoshuhudia mkoani humo kama za Viwanda, Madini, Ufugaji, Uvuvi pamoja na Utalii.
"Ndugu zangu wageni Mkoa wa Mwanza una idadi kubwa ya Mifugo na pia sehemu kubwa ya ziwa Victoria ipo Tanzania hivyo unapotaka kuwekeza kwa upande wa usindikaji wa nyama au ngozi au Ufugaji wa kisasa wa samaki Mwanza ni eneo mwafaka kabisa", amesema Machunda wakati akitoa taarifa fupi ya Mkoa huo kwa wageni hao kutoka Jimbo la Jiangsu.
Ameongeza kuwa Tanzania na China ni Mataifa ndugu na marafiki kwa miaka mingi , uhusiano ambao uliasisiwa na viongozi wa zamani wa nchi hizi Hayati Julius Nyerere na Mao Tsetung na kufanya raia wa pande hizo mbili kuzidi kufaidika kwenye sekta mbalimbali.
Akizungumzia ziara ya wageni hao Mkuu wa Idara ya viwanda, biashara na uwekezaji Patrick Karangwa amesema Mkoa wa Mwanza unazidi kupata umaarufu kutokana na mvuto wake wa kuwekeza hivyo wageni hao wamepata wigo mpana kabla ya kufika rasmi Gavana kutoka jimboni kwao.
"Kama alivyotangulia kusema Kaimu Katibu Tawala, wageni hawa watapata fursa ya kujionea miradi mbalimbali inayokwenda kuimarisha uchumi wa mkoa huu na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, huu ni mwanzo mzuri wa safari ya uwekezaji". Karangwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.