Wakuu wa Shule za Sekondari Mkoani Mwanza (TAHOSSA) wamefanya kikao katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bwiru wakiwa na lengo la kuleta umoja na kujadili kuhusu maendeleo ya taaluma Mkoani hapo.
Akiongea katika kikao hicho Mgeni rasmi ambaye ni Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Michael Ligola amesema, ili kukuza taaluma ni lazima kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kuaminiana na kuwa na nidhamu katika kazi kwa kuepuka udanganyifu na kutokujihusisha na siasa.
"Lugha nzuri kwa wasaidizi na wazazi wanaokuja kufuatilia maendeleo ya watoto huleta amani na ushirikiano katika kazi,hii huleta picha nzuri kwani hujenga uaminifu,"alisema Ligola.
Aidha aliongeza kuwa nidhamu ya wanafunzi imeshuka sana na hii ndiyo inayopelekea baadhi ya shule kuto faulu vizuri katika masomo, na kuwaasa wakuu hao kuhakikisha wanasimamia nidhamu ya wanafunzi na walimu pia.
"Hatupo katika kuhakikisha watoto wanafukuzwa shule, walimu wa malezi kwa namna moja ama nyingine, wajitahidi kurudisha nidhamu ya wanafunzi na kuhakikisha kuwa utoro unadhibitiwa pia walimu wanaokiuka taratibu wachukuliwe hatua.
Ligola amewataka wakuu wa shule kuwaamini na kuwaandaa wasaidizi wao kuwa wakuu wa shule na viongozi wazuri wa baadaye katika Nchi hii.
Hata hivyo ameongeza kuwa ili kuendelea kufanya vizuri katika taaluma ni vema kufanya majaribio mara kwa mara, na amewahakikishia kuwa Serikali inafahamu changamoto wanazokumbana nazo walimu na inaendelea kuzifanyia kazi.
"Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyampulukano Christine E. Zegela amesema mara nyingi wao wamefanikiwa kwa sababu pale mwanafunzi anaposhindwa kufaulu wanakaa naye kujua tatizo ni nini pia wanawaita wazazi ili kushauliana namna ya kuboresha elimu, hata hivyo walianzisha chakula shuleni hii imeboresha ufaulu kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana Nganza Yasinta Lyimo amesema kuwa nidhamu kwa walimu na wanafunzi ndiyo msingi wa ufaulu katika shule yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.