Watendaji na viongozi wa ngazi zote Mkoani Mwanza wametakiwa kuwajibika vilivyo ili kuongeza hamasa kwa wananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini novemba 24 mwaka huu.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa mwanza Mhe.John Mongella wakati akizungumuza na wakuu wa wilaya nawatendaji wa halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza pamoja na kamati za ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya ili kujadili mikakati mbalimbali itakayofanikisha uchaguzi huo bila dosari.
“Sasa tupo tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa ambao utatupatia viongozi wa wananchi ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa, lakini kumekuwa na tatizo la ushiriki duni kwa wananchi wetu labda kutokana na uelewa hafifu juu ya umuhimu wa chaguzi hizi.
“Sasa ninawaagiza watendaji wote mkawajibike kuhakikisha mnaongeza hamasa kwa wananchi wetu ili wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi huu hasa kwa kuanza na kujiandikisha kwenye daftari la wakazi na wananchi ili wapate sifa ya msingi kabisa cha kushiriki uchaguzi huu ili kuimarisha demokrasia.
“Kwani kwa mfumo wa nchi yetu demokrasia inaambatana kabisa na mchakato wa maendeleo na mfumo wa ulinzi na usalama, ndiyo maana katika ngazi husika viongozi hawa watakaochaguliwa ndiyo wanatambulika kama viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao.
“kwa hiyo nitumie fursa hii kuwaelekeza viongozi wote kwenye mkoa, wilaya hadi ngazi ya vitongoji kukahakikisha tunatengeneza hamasa ya kutosha ili wananchi wetu wajiandikishe, pia tunajenga hamasa kwa viongozi wa kijamii na wao wasiwe nyuma katika hili.
“Lakini pia pamoja na hayo wote tunaohusika na kamati ya ulinzi na usalama tuhakikishe zoezi hili linafanyika kwa amani kwenye maeneo yote kuanzia zoezi la uandikishaji hadi kupiga kura, na yeyote atakayeonekana kuvuruga mchakato huu achukuliwe hatua mara moja kwani huu ni kama mwanzo wa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka kesho,”alisema Mongella.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa wilaya wengine, Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Mhe.Emmanuel Kipole amesema kuwa maagizo ya Mkuu wa Mkoa ni ya msingi na yanatekelezeka hasa ukizingatiwa kuwa yanalenga kuleta tija na kufanikisha adhima ya kupata viongozi bora bila kupoteza amani ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
“Maagizo haya ni muhimu kwani uchaguzi tunaouendea wavitongoji na vijiji ndiyo chimbuko la serikali za mitaa na ndio msingi wa maendeleo kwa maeneo hayo kwani ina machango mkubwa katika kushirikiana na serikali kuu ili kufanikisha utekelezaji wa sera mbalimbali.
“Hivyo sisi kama wakuu wa wilaya ikiwemo mimi ni lazima tuwahamasishe wananchi kushiriki uchaguzi huu kwa maana serikali ya mtaa ndio serikali iliyo karibu zaidi na wao na inayoweza kujionea kwa macho matatizo wanayokutana nayo na pengine kuyatatuia kabla ya serikali kuu.
“Lakini pia nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi wa wilaya yangu na mkoa wa mwanza kwa ujumla kuacha kufanya uchaguzi huu kwa mazoea kwani kuna maeneo unakuta viongozi ndiyo walewale ambao kwa muda mrefu wameshindwa kupeleka mbele sera na dhamira ya maendeleo, sasa kila mmoja ashiriki kikamilifu ili kwa tupeleke maendeleo mbele,"alisema Kipole.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.