Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amezitaka Halmashauri mkoani humo kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kujihakikishia makusanyo yanayokidhi na kuweza kufikia makisio ya bajeti za Halmashauri zao kwa mwaka 2023/24.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Januari 23, 2023 wakati wa Mkutano wa Majumuisho ya ziara yake aliyoifanya mapema mwezi huu kwa kuzitembelea Halmashauri zote mkoani humo kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na ukaguzi wa Miundombinu ya vyumba vya Madarasa.
Amesema mazao kama Dengu na Choroko yanaweza kusaidia sana kukuza kipato cha Halmashauri hasa Magu ambayo ardhi yake ni rafiki kwa kilimo cha mazao hayo lakini Halmashauri imekua haiwapi kipaumbele kwenye ukusanyaji wa mapato hadi kufikia hatua ya kunufaisha Mikoa ya jirani hivyo ni lazime wawe na mkakati wa kuboresha eneo hilo.
"Kwa namna tulivyojipanga kuikuza Mwanza basi tuna safari yenye gharama sana katika kufanikisha malengo, naomba kila mmoja wenu akapitie upya makadirio ya makusanyo ya ndani na waheshimiwa wakuu wa Wilaya mkasimamie ili tupate uhalisia wa kiasi gani Mkoa wa Mwanza utakusanya kwenye mwaka ujao wa fedha." Mhe. Malima.
Aidha, amekemea tabia ya ufuatiliaji hafifu wa marejesho yatokanayo na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kisheria kwenye makundi ya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu kutoka makusanyo ya mapato ya ndani hali inayopelekea pesa nyingi kuwa nje na kuwanyima fursa wengine wanaohitaji kukopeshwa.
Vilevile, amezitaka Halmashauri kuacha tabia ya kutengeneza vikundi vya kirafiki au vikundi hewa kwa madhumuni ya kujipatia kipato kisicho halali bali ni lazima wafanye kazi hiyo kwa uzalendo mkubwa ili kuipa jamii ustawi kwani ndio adhma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bila kikwazo, Mhe. Malima ameziagiza Halmashauri zote kuweka bajeti ya kutosha kununua taulo za kike na kwamba katika utekelezaji wa hilo ni lazima wahakikishe wanazigawa kwa wakati kwani wanafunzi wa kike wakikosa zana hizo husabanisha tabia ya utoro kwa kujisia unyonge na inawajengea hofu.
"Najiweka kwenye nafasi ya kuhakikisha tunajiweka pamoja kama Menejimenti ya Halmashauri ili kuhakikisha mapato ya ndani yanakua na kwa Idara yangu ya Elimu Sekondari nitahakikisha wanafunzi wanapata Elimu bora ili kutimiza adhma ya serikali kwa wanafunzi." Amesema Genoveva Chuchuba, Afisa Elimu Sekondari kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.