Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewaagiza Halmashauri ya Buchosa kuhakikisha ndani ya Siku Tisini wanaendeleza Miradi mbalimbali iliyokwama katika maeneo tofauti kwenye Halmashauri hiyo kwa fedha za mapato ya ndani kwa mujibu wa sheria.
Ametoa agizo hilo mapema leo kwenye Baraza Maalumu la Madiwani la kujadili Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa 2020/21 na kubaini kuwa fedha za Mapato ya Ndani hazielekezwi kwenye Miradi ya maendeleo kinyume na sheria inavyotaka na badala yake zinatumika kwa shughuli za Utawala.
"Nikiwa kwenye Mkoa huu hakuna hoja ambayo itakosa majibu hata kumfunga mtu au kumfilisi ni majibu, naleta timu maalumu kuchunguza Halmashauri hii ili tujiridhishe kupata thamani ya miradi na tukipata viashiria vya ubadhirifu tutaenda mbele zaidi ya hapo nanyi Waheshimiwa Madiwani msikae kimya mnapoona dalili mbaya." amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
"Tayari tuna maelekezo kutoka TAMISEMl kwa wanaoshindwa kujibu hoja na tutaanza na hapa Buchosa, anayeshindwa kujibu hoja na anayesababisha hoja lazima tuwachukulie hatua na tutaleta wataalamu waje kuwawezesha waheshimiwa madiwani kwenye eneo hili." amesema Katibu Tawala wa Mkoa, Ndugu Ngusa Samike.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amebainisha kuwa awali Halmashauri hiyo ilikua na tatizo la Utendaji kwenye Kitengo cha Ukaguzi wa ndani lakini wamelitatua hilo na amemuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa Buchosa itabadirika kwa kufuata taratibu na kanuni za fedha.
"Tumekua tukipokea fedha za miradi ila menejimenti haizingatii na kuacha miradi inakwama kama Zahanati ya kijiji cha Nyashana walifanya hivyo na kwakweli nawambia wataalamu lazima wabadilike na Mkurugenzi simamia haya na tutachukua hatua." amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Buchosa, Mhe. Idama Kibanzi.
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani amesema kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2020/21 Halmashauri hiyo wamekua na jumla ya hoja 55 na kwamba kati ya Hoja 37 za 2020/21 ni 3 tu zimejibiwa kutokana na menejimenti kutoweka mkakati thabiti wa kujibu Hoja kikamilifu.
"Nashauri Wakuu wa Idara kuwa na Ushirikiano maana kuhusu ujibuji wa hoja kuna mapungufu makubwa kwenye Halmashauri hii na ndio maana tumeona kwenye hoja za nyuma hakukua na majibu ya pamoja ya menejimenti bali kila mkuu wa idara amekua akisema lake yaani hakukua na Mawasiliano mazuri." Amebainisha.
Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Abiud Sanga amesema Halmashauri ya Buchosa wamekua wakisuasua kwenye kufuata ushauri na kusababisha kuendelea kubaki na hoja nyingi hata baada ya kutoa ushauri wa namna ya kuziondoa.
"Tuna maboma matano wananchi wamejenga kwenye shule ya Sekondari Katoma pamoja na ujenzi wa nyumba ya Walimu ya mbili kwa moja ila serikali haiyamalizii maboma hayo, tunaiomba Halamshauri kuyaokoa maboma haya ili watoto wapate shule jirani na kwao wapunguze umbali wa kutembea zaidi ya KM 10." Amesema Mhe Isack Mashimba, Diwani wa Kata ya Kalebezo.
_Mwisho_
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.