Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewataka Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa Elimu kwa Wadau wa Usafirishaji juu ya Sheria ndogo ya Tozo za Vyombo vya Usafiri katika Vituo vya Mabasi Ili kuongeza wigo wa Makusanyo.
Mhe. Gabriel ametoa agizo hilo leo Juni 21, 2022 wakati Baraza la Madiwani lililokutana kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo mahsusi kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021.
"Tumeona kwenye Ushuru wa Hoteli tumetoza kwa asilimia 27 tu, yaani maana yake ni kwamba tumeshindwa kutoza kwa asilimia 73, tunahitaji kuongeza nguvu na kufanya utafiti kwenye suala la kodi ili tuisogeze mbele Halmashauri yetu." Amesema.
"Wanasheria watano ni wengi mno mnaweza mkajipanga kufanikiwa vizuri kwenye hili na hapa naona mchakato wenu wa nyuma umenasa na hoja imekataa kutoka, sasa nawapa wiki tano mkatoe Elimu ya Tozo za Vyombo vya Usafiri katika Vituo vya Mabasi tena muanze kutoa Elimu hapa ndani" amesisitiza.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali Athuman Mustapha ametoa wito kwa watumishi wa Halmashauri hiyo kufuata sheria, taratibu na kanuni za fedha ili kujiepusha na hoja zinazoepukika.
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhe. Costantine Sima amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kuanzia sasa Halmashauri hiyo itasimamia kwa umakini zaidi kutatua changamoto zilizoibuliwa na ripoti hiyo. "Wingi wa hoja sio sifa, tunakwenda kusimamia kwa dhati kutatua yote yanayosababisha kutuingiza kwenye hoja hizi."
Ndugu Sekiete Yahaya, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza amesema kutokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ya kuishia Juni 2021, hoja za Miaka ya nyuma zilikua zimebaki 71 ambapo 37 zilifungwa na 5 zimefungwa kwa kupita wakati hivyo hoja za miaka ya nyuma zimebaki 29 ambazo zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
"Mhe. Mwenyekiti, Halmashauri ya Jiji la Mwanza iliwasilisha taarifa zake za fedha na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya Ukaguzi ambapo Halmashauri imepata Hati safi kwa miaka ya fedha mitano mfululizo ambayo ni kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21." amefafanua Mkurugenzi.
_Mwisho_
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.