Halmashauri zilizopo Kanda ya ziwa zatakiwa kuhakikisha kamati za Fedha zinajengewa Uwezo
Halmashauri za Mikoa ya Kanda ya ziwa zimetakiwa kuhakikisha Kamati za Fedha, Uongozi na Mipango zinapatiwa mafunzo ili kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani wa kamati hizo kuzisimamia Halmashauri zao kwa ufanisi.
Agizo hilo limetolewa leo tarehe 19 Septemba 2023 na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Miundombinu, Mbunifu Majengo Chagu Nghoma kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza wakati akifungua mafunzo ya Kamati hizo yaliyoandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi TAMISEMI.
Amesema, ili ipatikane tija kwenye utekelezaji wa majukumu ya kamati hizo Mhe. Makamu wa Rais kupitia Mkutano wa 37 wa ALAT uliofanyika Mwezi Mei mwaka huu aliagiza kupatiwa mafunzo elekezi kwa kamati hizo lakini kumekua na uzembeaji wa kushiriki mafunzo yanayoandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa jambo ambalo halikubaliki.
Chagu amefafanua kuwa, ili waheshimiwa Madiwani waweze kuzisimamia vema Halmashauri zao hususani taratibu, kanuni na sheria za usimamizi wa fedha ni lazima wajumbe wa Kamati hizo wajengewe uwezo mara kwa mara wa juu ya msingi wa kisheria wa uwepo wa kamati hizo na majukumu yake hivyo, Halmashauri hazipaswi kubaki nyuma kwenye hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo), Mkuu wa Kampasi ya Shinyanga (SHYCA) Dkt. John Kasubi amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuzijengea uwezo kamati hizo ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwenye Halmashauri zao.
Aidha, amefafanua kuwa mafunzo hayo yanayoendelea kwa wakati mmoja kwenye Mikoa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kati na Ziwa ni muendelezo wa utekelezaji wa agizo la Mhe. Makamu wa Rais kwani tayari yalishatolewa kwenye Kanda ya Kaskazini na Mashariki na kwamba Chuo cha Serikali za Mitaa ndio Chuo kiongozi katika kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa na ndio wafundishaji wa mafunzo hayo.
Vilevile, Dkt. Kasubi ametumia wasaa huo kuwakaribisha wananchi kuwapeleka vijana wao kujiunga na chuo hicho katika kampasi zake zilizopo Hombolo, Dodoma mjini na Shinyanga kilichopo Kanda ya Ziwa mkoani Shinyanga ili waweze kupata elimu katika ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada katika fani mbalimbali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.