Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema huduma za maji mkoani humo zimeanza kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) na Shirika la Ugavi (TANESCO) kurekebisha tatizo.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Sptemba, 2025 kwenye Chanzo cha Maji cha Butimba wilayani Nyamagana alipofika kufanya ukaguzi kwenye mitambo ya kuzalisha na kusambaza maji ambayo ilipata hitilafu takribani siku nne zilizopita.
Mhe. Mtanda amesema mafundi wamefanya kazi mchana na usiku kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kama kawaida na wamefanikisha hilo kwa kurejesha mawasiliano ya umeme kwenye pampu ya kusambaza maji kutoka kwenye chanzo hicho kwenda kwenye matenki.
“Changamoto iliyojitokeza hapa ni umeme kutofika kwenye pampu yaani kilichokua kimekwama ni mawasiliano ya umeme kufika kwenye pampu lakini kwa juhudi na ushiriniano wa wataalamu wetu napenda niwaambie wananchi kwamba tayari kazi ya matengenezo imekwisha.” Mhe. Mtanda.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwashukuru wataalamu wa Mamlaka hiyo ya Maji pamoja na TANESCO kwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mitambo inarejea katika hali ya kawaida na kwa kuweka mfumo ambao hautoruhusu mitambo ya maji kuathirika na hitilafu ya umeme endapo litatokea.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amewashukuru wataalamu kutoka wizara hiyo kwa kushirikiana na MWAUWASA pamoja na TANESCO kwa kufikisha nishati ya umeme kwenye pampu kama awali.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa, kwakweli mafundi na wataalamu wetu wamefanya kazi kubwa na niwakikishie tu wananchi kuwa tumewasha pampu na sasa wananchi tayari wameanza kupata huduma ya maji kama ilivyokua siku za nyuma.” Katibu Mkuu
Mbali ya hayo Mhe. Mkuu wa Mkoa akiwa ameambatana na Katibu Mkuu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA walihitimisha ziara kwa kuwatembelea Kiwanda cha Dawa, Zahanati na kwenye Makazi ya wananchi wa Buhongwa ambapo wamejiridhisha kwamba Maji yanatoka tena kwa kasi inayotakiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.