Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameunda kamati ya watu watano itakayoongozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo kufanya Uchunguzi kwenye utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa inayojengwa wilayani Ukerewe kufuatia malalamiko ya uwepo wa ubadhirifu wa fedha kwenye mradi huo.
Waziri Ummy amebainisha hayo leo jumatano disemba 21, 2022 wakati wa ziara yake Wilayani Ukerewe alipofika kukagua mwenendo wa ujenzi wa mradi huo kufuatia agizo la Mhe. Makamu wa Rais alipofanya ziara yake wilayani humo Novemba 25, 2022 na kumtaka Waziri wa Afya kufika kukagua mwenendo wa Ujenzi kutokana na malalamiko ya wananchi.
"Niseme wazi, kwa macho mimi nimeona kuwa gharama za Ujenzi kwenye mradi huu zipo juu na haziendani kabisa na thamani ya fedha zilizolipwa hakuna Bilioni 2.9 pale, hivyo naunda timu yangu ambayo itaongozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambayo itachunguza malalamiko ya wananchi wa Ukerewe kwenye mradi wao." Mhe. Ummy.
Amefafanua kuwa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa Ukerewe uliasisiwa na Mhe. Waziri Mkuu alipofika wilayani humo na kubaini uhitaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ili wananchi wa Ukerewe wasisafiri tena kwenda Sekou Toure au Bugando lakini watekelezaji wameamua kuiboresha hospitali ya Wilaya badala ya kujenga hospitali mpya ambayo ingejumuisha huduma za kibingwa za matibabu zinazoendana na miundombinu.
"Kama hili jengo la Kliniki ya Mama na Mtoto ni lanini hapa wakati hata kwenye Hospitali zingine tunaziondoa, hamjanishawishi kuwa baada ya Ujenzi huu wanaukerewe watapata huduma za kibingwa hapa hivyo hatujatatua tatizo maana huduma zinazotolewa hapa bado zipo kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo inatumika na mwanamke ambaye atafika hapa na matatizo makubwa ya uzazi bado hatosaidiwa hivyo ni lazima tutafakari hilo na tujielekeze huko." Mhe. Waziri amefafanua.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amesema kuwa kumekua na makosa tangia hatua za awali katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo kwa kutofuata taratibu za malipo, kutekelezwa kwa kuchelewa na miundombinu kutozingatia mahitaji halisi ya wananchi kwenye huduma za kibingwa.
"Rais Samia hata ukimwangalia machoni anaonesha ana dhamira ya dhati ya kutaka wananchi wake wapate huduma za kijamii na ndio maana analeta fedha kwenye miradi hivyo basi ni wajibu wetu kutekeleza miradi kwa mujibu wa sheria na wizara yetu haipo tayari kuona mtu hatimizi wajibu wake pasipo kuchukuliwa hatua." Mhe. David Silinde, Naibu Waziri TAMISEMl.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalage alifafanua kuwa baada ya Serikali kuona jiografia ya Kisiwa hicho na mahitaji kuwa makubwa ni vema ikipandishwa hadhi kuwa ya Rufaa ya Mkoa ndipo Mhe. Rais alitoa Shilingi Bilioni 2.69 kwa ajili ya kuanza ujenzi ambapo kwa sasa umefikia asilimia 62 ya utekelezaji.
Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Mhe. Joseph Mkundi amesema kwenye utekelezaji wa mradi huo wananchi wa Ukerewe wanakwazwa na mpango wa Miundombinu ya majengo, ucheleweshaji wa Ujenzi huo na thamani ya mradi kuonekana kuwa chini ya fedha zilizolipwa kwa Mkandarasi na ametoa wito kwa wizara kusaidia kupata suluhu ya jambo hilo ili mradi ukamilike.
"Katika wilaya yetu ya Ukerewe tuna visiwa 38 wananchi na wanawake wenzangu kwenye visiwa hivyo wanapata shida sana ya huduma za uzazi, nikuombe tupate vituo vya afya kwenye visiwa vikubwa ili wananchi walio wengi wapate huduma za Afya bila kusafiri umbali mrefu kuja kwenye Hospitali ya wilaya." Mhe. Furaha Matondo, Mbunge viti Maalum.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.