Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ndugu Balandya Elikana amewataka wajumbe wa kamati ya ulinzi wa wanawake na watoto (MTAKUWWA) mkoani humo kushirikiana na serikali kuhakikisha wanatambua na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili makundi hayo na kuwaondoa kwenye ukatili.
Ndugu Balandya amesema hayo leo Agosti 13, 2025 wakati akizindua mafunzo ya siku tatu kwa kamati ya Mkoa ya kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto NPA-VAWC 2024/25- 2028/29 II.
Amesema ni lazima mwanakamati azunguke kwenye jamii ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakwamisha katika kushiriki kwenye kujenga uchumi wao na kuhakikisha wanaweka misingi ya kuondoka changamoto hizo.
"Ukatili kwa wanawake na watoto unazuia maendeleo kwa jamii na nchi kwa ujumla kwani serikali inalazimika kuahughulika na majeraha ya ukatili kama kutibu na kunasihi, hivyo wajumbe nawaomba mkatekeleze wajibu wenu." Amesema Balandya.
Ameongeza kuwa mchanganyiko wa wajumbe kutoka kwenye taasisi na madhehebu ya dini mbalimbali umelenga kuyafikia makundi mbalimbali na kuhakikisha jamii yote inafikiwa na kupatiwa elimu dhidi ya ukatili.
Akizungumzia watoto wanaoishi mtaani, Katibu tawala amesema kila mmoja kwenye eneo lake ahakikishe anafikisha ujumbe kwamba ni vibaya kuwahudumia watoto wanaoomba pesa mtaani kwani inapelekea kuwafanya waendelee kuwepo.
Akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Gabriel Mashauri amebainisha kuwa kwa siku tatu wajumbe watapitishwa katika maeneo 8 ambazo ni afua za kufuata na mwisho wa mafunzo hayo kila mjumbe atajua majukumu yake ya kila siku katika kuhakikisha watoto na wanawake wanakingwa na ukatili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.