Jumla ya watoto 846,733 waliochini ya miaka 5 mkoani Mwanza wanatarajia kupata chanjo ya matone (POLIO) ili kuwajengea kinga na kuzuia kuenea kwa virusi hivyo .
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa chanjo Mkoa wa Mwanza Amos Kiteleja katika mkutano wa baraza la biashara Kati ya Sekta ya Umma na Binafsi uliofanyika leo Jijini Mwanza.
Ameeleza kuwa kampeni hiyo inachangiwa na nchi kuwa katika hatari ya ugonjwa huo kuingia mara baada ya February 17 mwaka huu nchi ya Malawi kutoa tamko la kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo nchini humo baada ya mtoto mmoja kutoka Mji Mkuu wa Lilongwe kudhibitika kuwa na ugonjwa huo.
" Nchi ya Malawi na Tanzania kuna mwingiliano mkubwa wa kibiashara na huduma nyingine za kijamii hivyo hatari ipo na chanjo ni muhimu itasaidia kuzuia ugonjwa huo usienee kwani kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata mgonjwa wa Polio Julai 1996 hivyo kampeni hii inatarajiwa kufanyika katika nchi zinazopakana na Malawi ikiwemo Zambia,Msumbuji, Zimbabwe na Malawi yenyewe" anaeleza Kiteleja.
Anaeleza kuwa kampeni hiyo itaanza April 28 hadi Mei 1 mwaka huu watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano watachanja bila kujali chanjo alizopata siku za nyuma ambapo Halmashauri ya Ukerewe watafikiwa watoto 108,937, Magu 93,721, Nyamagana 92,698, Kwimba 134,636, Sengerema 108,597, Ilemela 85,834, Misugwi 116,167 na Buchosa 106,143 .
" Jamii itambue kuwa mtoto ata kama alichanjwa jana lakini zoezi likianza atachanjwa tena chanjo hizi ni salama na katika zoezi ili kadi za watoto hazitatumika lakini kila baada ya mtoto kuchanjwa atawekewa alama maalum kwenye kidole kidogo cha mkono " anaeleza na kuongeza kuwa
"Kampeni hii ya siku nne itakuwa ni nyumba kwa nyumba na vituo vya muda vitatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo masoko, shule,misikiti,makanisa,mashambani,vituo vya mabasi ,makambi ya wavuvi pia vituo vya kudumu timu za uchanjaji zitakuwa kwenye vituo vya kutoa huduma za afya kwa siku hizo." anaeleza Kiteleja.
Aidha ameeleza kuwa ugonjwa huo hauna tiba ila hukingwa na chanjo ya Polio ambayo ipo katika mfumo wa matone na sindano pia unapompata mtu hushambulia mishipa ya fahamu,kupooza na hatimaye kifo na unaweza kumpata mtu yeyote katika umri wowote ila mtoto huathirika zaidi .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriel aliitaka jamii kuipokea na kutokuwa na hofu bali itambue chanjo ni ileile inayotumika miaka yote lengo ni kuongeza kinga , kuzuia mlipuko na kuwa Taifa lenye afya njema na kuwa na uchumi imara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.