Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe.Dkt. Stergomena Tax amewasili jijini Mwanza kwa ziara ya siku mbili huku akishangazwa na namna mkoa huo ulivyobadilika kwa shughuli za maendeleo kitendo kinachoashiria kukua kwa uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja.
Dkt. Tax amewasili Mwanza akitokea jijini Dar es Salaam na kupokelewa na viongozi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kufanya kikao kifupi kabla ya kuendelea na ziara Wilaya ya Magu ambapo alisema ameshangazwa na namna mkoa huo ulivyobadilika kwa muda mfupi.
Alisema alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ameshuhudia maboresho makubwa yakiwamo upanuzi wa barabara ya kurukia ndege, jengo la mzigo na mnara wa kuongozea ndege na majengo mengine makubwa mitaani jambo ambalo linadhihirisha wazi Serikali imekusudia kuimarisha uchumi wa nchi na wananchi wake.
Dkt. Tax ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Mwanza, alisema kila anapobahatika kufika Mwanza anashuhudia mabadiliko makubwa ambapo aliwataka viongozi waliopewa dhamana kuendelea na kaai hiyohiyo ili makusudio ya Rais Mhe. Dkt. John Magufuli yaweze kutimia ndani ya miaka atakayotawala.
“Mwanza ni jiji kubwa na hivyo linastahili kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa kama SADC, binafsi nimefarijika kuona mabadiliko yanayoonekana kwa macho kuanzia uwanja wa ndege hadi huku mitaani, majengo ya kisasa ambayo awali tulikuwa tunayaona kwingineko lakini leo tunayaona hapa,"alisema Dkt.Tax.
“Naomba viongozi muendelee kwa kasi hiyo hiyo ya kusimamia shughuli za maendeleo ili wananchi waweze kufaidi utumishi wenu chini ya utawala wa Rais Dkt. Magufuli, taifa limepata kiongozi ambaye ana uchungu na watu wake na rasilimali za nchi hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake,”alisema.
Awali, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emil Kasagara alimshukuru Dk. Tax kutembelea Mwanza huku akimpongeza namna anavyoiwakilisha Tanzania na kuongoza vizuri mkutano wa SADC uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
“Tunashukuru kwa ujio wako mkoani kwetu na tunasema karibu sana, tunafarijika kwa nafasi yako ndani ya SADC na jinsi unavyoiwakilisha nchi katika mikutano mbalimbali, hivyo ni fahari kwetu kuona Tanzania tukipokea kijiti cha uenyekiti, bila shaka tutafika salama ndani ya mwaka mmoja na kutimiza maazimio mliofikia,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.