Katibu wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba amewatahadharisha waombaji wa ajira nchini dhidi ya vitendo vya utapeli vinavyoendelea kujitokeza, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu, mtumishi au msimamizi wa usaili mwenye uwezo wa kumpatia msailiwa ajira kwa njia ya mkato.

Akizungumza wakati wa ufuatiliaji wa zoezi la usaili kwa waombaji wa ajira katika Mkoa wa Mwanza, Katibu huyo amesema ajira zote zinazotangazwa na Serikali hazijamlenga mtu binafsi, kundi au eneo fulani, bali ni kwa Watanzania wote wenye sifa na vigezo, ambapo nafasi hutolewa kwa misingi ya ushindani wa haki.

Amesema kuwa Serikali imeweka mfumo madhubuti wa kuhakikisha mchakato wa ajira unazingatia haki, sheria, miongozo na utu, hivyo hakuna sababu ya waombaji kujihusisha na vitendo vya kutoa au kupokea fedha kwa lengo la kupata ajira.

“Juzi mzazi mmoja alifika ofisini Sekretarieti ya Ajira Dodoma akitokea Mkoa wa Mara, akilalamika kutapeliwa shilingi milioni nne kwa kuahidiwa ajira. Nashangaa mtu anatoa fedha ili apate ajira, kwani mwisho wa siku atatapeliwa na ajira hataipata kwa sababu hakuna mwenye uwezo wa kumpatia mtu ajira,”amesema Katibu huyo.

Katibu huyo ameeleza kuwa kwa sasa mchakato wa ajira unatekelezwa kwa kutumia mfumo wa kidijitali, ambapo hatua zote muhimu ikiwemo upakiaji wa vyeti, ujazaji wa taarifa binafsi na usaili wa kuandika hufanyika kupitia mtandao, isipokuwa hatua ya usaili wa mahojiano kwa waombaji watakaofaulu hatua za awali.

Katika kuondoa wasiwasi kwa waombaji, Kiongozi huyo amesema mfumo huo ni rafiki na rahisi kutumia, na kuwahimiza wale wasio na ujuzi wa kutumia kompyuta kutoona aibu kuuliza au kuomba msaada wanapokumbana na changamoto.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Daniel Machunda, amesema maandalizi ya usaili yamezingatia kikamilifu masuala ya usalama, utulivu na uwepo wa wataalamu wa kutosha.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.