Ukara ni miongoni mwa msururu wa visiwa vilivyo katika ziwa Victoria upande wa Tanzania, visiwa vingine ni Bumbile, Maisome, Iramba vikibebwa na kisiwa cha Ukerewe kwa kutaja baadhi.
Miongoni mwa visiwa hivi, Ukara ni kisiwa maarufu baada ya Ukerewe kwa idadi ya wakaazi wa asili, umaarufu wa biashara ya samaki, mhogo pamoja na mazao mengine ukiwemo ufugaji wa ng’ombe bora wajulikanao kama ng’ombe wa Ukara.
Kisiwa hiki pia ni maarufu zaidi kutokana na kuwa na wingi wa wasomi pia juhudi na uchapakazi wa hali ya juu ya wakazi wake.
Kisiwa cha Ukara kina kata nne za Bwisya, Nyamanga, Bukungu na Kome ambavyo vina jumla ya vijiji vinane vyenye jumla ya wakazi wanaokisiwa kufikiwa 55,000 kwa maoteo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Kisiwa hiki kina kituo cha Afya kimoja na zahanati tatu zinazofanya kazi. Zahanati hizi ni Chifule, Nyamanga na Bukiko. Aidha zahanati zingine tatu ziko katika hatua ya ujenzi
Uvuvi ni msamiati ambao sio tu kwamba haufahamiki kwa wakazi wa Ukara, bali pia haukubaliki kabisa katika mila na desturi zao, zinazouona uvivu kama kikwazo cha kuwaletea maendeleo endelevu.
Mwaka mmoja uliopita, Ukara, wilaya ya Ukerewe, mkoa wa Mwanza na kanda ya ziwa kwa ujumla, zilikumbwa na balaa la kutisha baada ya kupinduka na kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere na kusababisha watu 300 kupoteza maisha.
Ajali hiyo iliyotokea Septemba 20 mwaka 2018, ilisababisha idadi kubwa ya pili katika ajali zilizopata kutokea katika ziwa Victoria ikitanguliwa na ajali ya kupinduka na kuzama kwa meli ya Mv Bukoba.
Idadi kubwa ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo ya kivuko cha Mv Nyerere walitokea mikoa ya kanda ya ziwa, lakini Ukara peke yake iliongoza kwa idadi ya vifo vilivyotokea katika ajali hiyo.
Kuna simulizi ya kusikitisha kuwa karibu kila familia katika eneo la Ukara ilipata msiba.
Bwisya ni eneo lililoongoza kwa kupoteza idadi kubwa ya wananchi waliokuwa walipa kodi za serikali kwani wengi waliokuwa abiria waliofariki katika ajali hiyo walikuwa wafanyabiashara na wanunuzi wa bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika maeneo ya Ukara na maeneo jirani.
Historia ya ujenzi
Kuzama kwa kivuko hicho kulitatiza vilivyo shughuli na huduma za usafiri kwani Mv Nyerere ndicho kilikuwa kivuko pekee kilichorahisisha mawasiliano kati ya Ukerewe na Ukara.
Kwa kulifahamu hilo, kama kuna jambo kubwa na la maana ambalo serikali ililifanya kwenye kisiwa hicho ni kuwanusuru wananchi wa eneo lililopata ajali kwa kuanza kujenga miundommbinu ya afya, ikiwa ni pamoja na Kituo kikubwa cha afya chenye hadhi ya hospitali ya Wilaya.
Serikali haraka haraka ilianza juhudi za kukiibua kivuko hicho na pia kuangalia njia nyingine kwa ajili ya mawasiliano ya usafiri kati ya Ukara na maeneo mengine ya mkoa wa Mwanza na mikoa jirani.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, serikali ilibaini moja ya changamoto ya wananchi wa Ukara mbali ya usafiri na mawasiliano mengine, ilikuwa ni ukosefu wa huduma za uhakika za afya.
Hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya hapo, ilikuwa ni kuanzisha ujenzi wa kituo cha afya chenye hadhi ya hosipitali ambacho kwa sasa kimekamilika(kama kinavyoonekana pichani) katika eneo la Bwisya huko Ukara.
Fedha za ujenzi
Changamoto ya fedha za ujenzi wa kituo hicho cha kisasa zilimalizwa na uamuzi mahususi wa viongozi wakuu wa serikali chini ya usimamizi mahususi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella uliwezesha sehemu ya fedha kiasi cha Sh milioni 800 zilizotolewa kwa ajili ya rambirambi kuanzisha ujenzi wa kituo hicho cha Bwisya.
Kituo hiki kipya cha afya bila shaka ni miongoni mwa vituo bora vya afya nchini kwa kuzingatia haswa ubora na muonekano wa majengo yake na pia wingi wa majengo yenyewe.
Kwa kuzingatia sifa hizi, ndio maana nasema pamoja na kwamba kituo hicho cha Bwisya kilijengwa kama kituo cha afya, lakini pengine kutokana na hali na hadhi ya majengo yake na muonekano wake kwa ujumla, kumeshawishi viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kukitangaza kuwa hosipitali kamili.
Shughuli za pekee zimwendee Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela kwa kushirikiana na timu yake ya watendaji, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Kornel Maghembe kutokana na usimamizi wao murua, wamefanya kazi usiku na mchana kwa kushirikiana na timu ya watalaam wa ujenzi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kufanikisha ujenzi wa kituo hicho muhimu ambacho kitakuwa kinatoa huduma za afya kwa wakazi wa Bwisya na Ukara.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella anasema kazi ya usimamizi wa kituo hicho ilimnyima usingizi, ambapo anasema kwa kushirikiana na timu ya watalaam wa ujenzi, wasaidizi wake na wananchi wa Ukara sasa ujenzi wa kituo hicho umekamilika na kimeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Anasema fedha hizo zaidi ya Sh milioni 800 zimetumika kujenga jumla ya majengo 11, nyumba za watumishi mbili, wadi ya wazazi, chumba cha upasuaji, kufulia nguo na ujenzi wa uzio katika eneo lote la hosipitali.
“Kwenye kituo hiki pia umejengwa mfumo wa maji tenki kubwa na pia kimewekewa mfumo wa sola,” anasema na kuongeza kuwa Kituo hicho cha Bwisya kitakuwa ni cha kiwango cha hosipitali ya wilaya.
Anamsahukuru Mhe. Rais Dkt.John Magufuli kwa moyo wake wa upendo na maelekezo aliyotoa ya kutumiwa kwa kiasi cha fedha Sh Milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kikubwa cha afya, ambacho kimeondoa adha ya matibabu kwa wakazi wa Bwisya na maeneo jirani.
Ikama ya watalaam
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa anasema Kituo cha Afya cha Bwisya ambacho pia kinatoa huduma za afya kwa wakazi wa visiwa jirani vya Sizu, Kweru na Irugwa.
Anasema kisiwa cha Ukara kina kituo cha Afya kimoja na zahanati tatu zinazofanya kazi. Zahanati hizo ni Chifule, Nyamanga na Bukiko. Aidha zahanati zingine tatu ziko katika hatua ya ujenzi ambazo ni Nyang’ombe, Chibasi na Kome.
Anasema Kituo cha Afya cha Bwisya katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano, kilipata ufadhili mkubwa wa kujengewa miundombinu ya majengo ya kutosheleza huduma zote kwa awamu mbili.
Anasema katika awamu ya kwanza kituo hicho kilipata jumla ya Sh milioni 400 ambazo zilitumika kujenga wodi ya wazazi, maabara, nyumba moja ya watumishi, jengo la upasuaji (theatre) na chumba cha kuhifadhia maiti.
Katika awamu ya pili, Dk Rutachunzibwa anasema kufuatia ajali ya kivuko cha Mv Nyerere, Rais Dk. John Magufuli alitoa fedha za rambirambi takribani Sh milioni 800 ili zitumike kuboresha kituo hicho.
Anasema fedha hizo zimetumika kujenga wodi tatu, jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma ya uchunguzi wa Radiolojia(x-ray/ultrasound), jengo la kufulia, nyumba za watumishi, tanki kubwa la maji na uzio wa kituo ambavyo kwa sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.
Dkt. Rutachuzibwa anasema kufuatia maboresho hayo, tayari halmashauri ya wilaya ya Ukerewe imepeleka Daktari mmoja na mtaalam wa kutoa dawa za ganzi wakati wa upasuaji ili huduma za upasuaji ziweze kuanza.
“Vifaa vya msingi vya kutoa huduma ya upasuaji tayari vimekwshapelekwa kwenye kituo hicho,” anasema.
Anasema serikali kupitia Bohari ya Dawa(MSD) inaendelea kuongeza vifaa vingine ili miundombinu yote iweze kutumika kikamilifu na kwamba ni mategemeo ya serikali ndani ya mwezi huu wa Julai huduma za upasuaji zitaanza rasmi.
Anasema kuanza kutolewa kwa huduma hizo za upasuaji katika kituo hicho cha Afya cha Bwisya kutapunguza adha ya rufaa ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kwa wagonjwa na watumishi.
Anaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutoa kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa mkoa wa Mwanza na maeneo mengine nchini.
Anasema kwa namna ya kipekee anatoa shukrani kwa Rais Dk John Magufuli kwa kutoa kipaumbele kwa Kituo cha Afya cha Bwisya kufuatia ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kwa madai kuwa fedha zilizotumika kuboresha kituo hicho angeamua hata zifanye marekebisho katika sekta nyingine.
“Lakini aliona sekta ya afya ni muhimu zaidi, hakika ameonyesha thamani kubwa katika sekta ya afya, na sisi watumishi tunaomsaidia tunaahidi kuchapa kazi ili mategemeo yake katika sekta ya afya yaweze kuonekana na wananchi wafaidike,” anasema Dk Rutachunzibwa na kumshukuru Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe na timu ya wajenzi kwa kazi kubwa waliyofanya kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Kornel Maghembe anasema ujenzi wa kituo hicho umekamilika na kwamba kwa sasa kimeanza kutoa huduma za tiba kwa wananchi wa ukara na maeneo ya vijiji jirani.
“Wananchi wa Ukerewe wana hamu kubwa ya kumuona Rais wetu mpendwa Dkt.John Magufuli anakuja kukifungua rasmi kituo hiki kwa sababu yeye ndiye aliyeleta fedha za ujenzi wa kituo hiki,” anasema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.