KUFUATIA MTAALA MPYA RAS MWANZA ATOA MAAGIZO KWA WATENDAJI SEKTA YA ELIMU
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amewataka watendaji sekta ya elimu kuhakikisha wanabadilika na kujifunza namna ya kutekeleza mtaala mpya ulioboreshwa ili waweze kuelewa na kutekeleza mabadiliko hayo yaliyoanza kutumika Januari 2025 kwa ufanisi katika Shule zao.
Ametoa agizo hilo mapema leo Jumatano Februari 05, 2025 Wilayani Sengerema wakati akifungua kikao cha Maafisa Elimu na wadhibiti ubora walioketi kutathmini utekelezaji wa shughuli za Elimu kwa mwaka 2024 na kuweka malengo ya kufanya vizuri zaidi.
Aidha, RAS Balandya amewataka kutathmini ubora na udhaifu wao na kuweka mikakati bora ya kufanya vizuri zaidi na kwamba wasibweteke kwa kuwa Mwanza imefanya vizuri kitaaluma katika mitihani yote hususani wa kidato cha nne ambapo ufaulu ni wa 98.2%.
Ili kuendelea kuwa bora, Ndg. Balandya amewataka wataalamu hao kuweka mikakati ya namna ya kukabili changamoto zinazorudisha taaluma nyuma kama wanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika pamoja na ufundishaji duni ili kubaki juu kitaaluma.
Pia amewataka maafisa hao kuweka mpango wa kufanikisha Mkoa kufanya vizuri zaidi kwenye michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA 2025 na kuendelea kusimamia fedha za ujenzi wa miundombinu bora ya elimu ambapo amebainisha kuwa mwaka 2024 Elimu Msingi imepokea zaidi ya Bilioni 24 na kwa sekondari Bilioni 17.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Mwalimu Martin Nkwabi amebainisha kuwa 2024 ulikua mwaka mzuri mathalani katika uboreshaji miundombinu, taaluma kwa mitihani ya upimaji na mitihani ya Taifa na hata katika michezo kwani Mwanza imeibuka kidedea.
Vilevile, amesema kiwango cha kuweka wanafunzi shuleni kimepanda kutoka 7% mwaka 2023 hadi 4% mwaka 2024 hivyo kiwango cha kuwafanya wanafunzi wadumu darasani ni kikubwa na kimefuta mdondoko.
Ujio wa mtaala mpya ulioboreshwa ni katika kutekeleza agizo la Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuboresha mitaala ya Elimu Msingi, Sekondari na Ualimu ili kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.