MKuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Senyi Ngaga kuendeleza kazi zilizokuwa zinafanywa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Mtemi Msafiri ikiwemo kukomesha mauaji ya kishirikina, kupambana na wauzaji na watengenezaji wa pombe haramu (gongo) na kuzuia uharibifu wa kukata miti na kuchoma mkaa bila kufuata taratibu.
Mhe.Mongella ameyasema hayo leo Agosti 16 mara baada ya kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya kwimba Mhe.Senyi Simon Ngaga katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
"Uende kuitafsiri nafasi uliyopewa na Mhe. Rais Dkt.John Magufuli kaendeleze vita dhidi ya mauaji ya kishirikina japo yamepungua ikiwezekana yaishe kabisa," alisema Mongella.
Mhe.Mongella aliongeza kuwa Kwimba ndiyo wilaya ya mwisho kimaendeleo Mkoani Mwanza kati ya Wilaya saba hivyo anahitaji aone mabadiliko ya kimaendeleo katika Wilaya ya hoyo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Ngaga ameomba ushirikiano kutoka kwa watumishi na wana mwanza kwa ujumla ili afanikishe malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Hata hivyo alikabidhiwa vitendea kazi ambavyo ni Katiba ya Jamuhuri ya vya Muungano wa Tanzania 1977,ilani ya uchaguzi wa Mwaka 2005,Sheria za Mitaa ya Mwaka 1977 pamoja na Masharti ya Mkuu wa wilaya ya Mwaka2016.
Awali Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika amesema anahitaji ushirikiano katika mahama kwa wananchi na watumiahi wote kwani wanaapa kuwa waadilifu.
"Viapo vikifuatwa mnakuwa watumishi wazuri,kwani ni uadilifu mkubwa, tumekusudia kuondoa kesi za muda mrefu na pia tumezindua kampeni katika Mkoa wa Geita,Mara na Mwanza ambao una misingi mnne itakayotusaidia katika Mahakama na wateja wetu,"alisema Mhe.Rumanyika.
"Haki yako Wajibu wangu, Napenda kesi nachukia Mrundikano, Kila mtu atende wajibu wake na Mrundikano wa Kesi ni Sumu ya Nchi"alisema Mhe. Rumanyika.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Mnec )wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Jamal Abdul Babu alisema kila mtu anastahili kutii Mamlaka iliyopo madarakani na utelekezaji wa ilani utasaidia watu wachape kazi.
Aidha Mhe.Mongella alisisitiza ukusanyaji wa mapato,utumiaji mzuri wa ardhi,kuwe na siasa safi, uongozi bora na kuwe na mkakati wa kuondoa umasikini hivyo italeta mshikamano na Maendeleo katika Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.