LENGO LA HOSPITALI ZA WILAYA NI KILA MWANANCHI APATE HUDUMA MAHALI ALIPO - WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu ww Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) amesema lengo la ujenzi wa Hospitali za Wilaya, Vituo vya afya na Zahanati ni kumuondolea usumbufu wa gharama na umbali mwananchi ili aweze kupata huduma mahali alipo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Mei 19, 2025 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Hospitali ya Wilaya ya Sengerema - Mwabaluhi ambapo amesema ziara ya kwenda hospitali hapo ilikuwa ni muhimu kwa sababu serikali inaweka msisitizo wa afya wa kule wananchi waliko.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema serikali imebeba jukumu la kubeba huduma ya vituo vya afya na kwa Sengerema vimeshajengwa vituo vya afya 6 na bado Serikali ina orodha ndefu ya vituo vya afya na amewahakikishia kuwa watavileta.
“Lengo la huduma hizi ni wanasengerema msipate adha ya kwenda umbali mrefu, na sio hapa tu kila sehemu serikali imejenga hospitali za wilaya”. Mhe. Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa rai kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo kuendelea kulinda vifaa vya Hospitali na kutoa taarifa pindi inapoonekana wale wasio waamifu wachache wanaotaka kuharibu taswira basi taarifa zitolewe haraka iwezekanavyo.
Akisoma taarifa ya mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Bw. Wilberd Bandola amesema mradi huo umekuwa ukitekelezwa kwa awamu na mpaka sasa Halmashauri imepokea kiasi cha shilingi 3,115,000,000 zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Hospitali.
Kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali hiyo kutawanufaisha wananchi wa Halmashauri ya Sengerema na maeneo jirani kupata huduma kwa urahisi na karibu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.