Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima anawakaribisha wananchi wote wa Mwanza na Mikoa ya Jirani kushiriki katika wiki ya kuzuia na kudhibiti Magonjwa yasiyoambukizwa itakayoanza Kitaifa kuanzia tarehe 05 -12 Novemba, 2022 kwenye Uwanja wa CCM Kilumba.
Wito huo umetolewa (Novemba 04, 2022) kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati Kiongozi huyo alipozungumza na Wadau wa Afya na Waandishi wa Habari ambapo amewasihi kutangaza kwa kina juu ya Maadhimisho hayo nyeti Kitaifa ili jamii ielimike kwa kufahamu asili na njia za kuepuka magonjwa hayo.
Mhe. Malima amesema, katika kipindi kisichozidi miaka tisa kumekua na ongezeko la kubwa la wagonjwa yasiyoambukizwa kama Kisukari, Shinikizo la juu la Damu, Magonjwa ya Moyo, Saratani, Pumu, Magonjwa ya Afya ya Akili na Ajali.
Ameongeza kuwa, moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya mtindo wa maisha ya watu kama ulaji usiofaa wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha mafuta, sukari, chumvi na ulaji mdogo wa matunda na mbogamboga pamoja na kutokufanya mazoezi na matumizi makubwa ya vilevi na tumbaku.
"Ongezeko la Magonjwa haya linaweza kuleta madhara makubwa kijamii, kiuchumi na kuhatarisha maendeleo ya nchi kutokana na kuongeza vifo vya mapema kwa wananchi ambao wangeweza kuchangia maendeleo na ongezeko la gharama za matibabu kutokana na gharama za matibabu."Amesema Mkuu wa Mkoa.
Malima amefafanua kuwa Maadhimisho hayo yataenda sambamba na matukio makubwa manne kama Tamasha la michezo litakalodumu wiki nzima, upimaji wa huduma za Afya, Kongamano la kisayansi litakalokutanisha wanasayansi na wabobezi mbalimbali wa huduma za Afya pamoja na hitimisho la wiki hiyo litalohusisha utoaji wa zawadi kwa washindi wa michezo.
Maadhimisho ya Wiki ya kuzuia na kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza itakayofanyika Mwanza Kitaifa iliasisiwa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) Waziri Mkuu wa Tanzania alipozindua Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukizwa mnamo tarehe 14 Novemba, 2019 na kutangaza wiki ya pili ya kila mwezi Novemba kuwa ni wiki Maalum ya suala hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.