MAAFISA BIASHARA NA MAENDELEO YA JAMII MUWE CHACHU YA MAGEUZI KWA WAJASIRIAMALI: RC MTANDA
Maafisa biashara na Maendeleo ya jamii kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa wametakiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa wajasiriamali kwa kutumia kikamilifu fursa zilizopo kwenye maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa leo Machi 4, 2024 Jijini Mwanza na Katibu Tawala Msaidizi Viwanda, Biashara na Uwekezaji Patrick Karangwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati wa ufunguzi wa Mradi wa kuwajengea uwezo wajasiriamali.
"Nimesikia hapa katika hotuba kuwa lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha vijana wanatumia utaalamu kwenye fursa zilizopo kama ni biashara za Dagaa, Nafaka au Ufugaji Samaki basi naomba uwe katika kiwango cha kumvutia mtumiaji wa mwisho," Karangwa.
Amesema Taasisi ya GS 1 inayotoa Mafunzo kwenye Mikoa mbalimbali imeanza na Kanda ya ziwa ikitambua uwingi wa fursa za kiuchumi zilizopo lakini kinachokwamisha ni namna ya kutumia utaalamu ili kuwepo na tija.
"Ziwa letu limejaa dagaa, lakini unawakuta wafanyabiashara wengi wanauza kwa kutumia visado badala ya kuwaweka vizuri kwenye vifungashio vya kisasa na vyenye mvuto", amesisitiza Karangwa wakati wa hotuba yake kwa Maafisa hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya GS 1 Bi. Fatma Kange amesema kwa muda mrefu ukosefu wa Msimbomilia (Barcodes) umeleta usumbufu kwa wafanyabiashara na kujikuta wakishindwa kupenya kwenye soka la ushindani, hivyo Serikali ikalazimika kuanza mchakato wa kuanzisha taasisi hii mwaka 2011.
"Ndugu mgeni rasmi taasisi za GS1 pamoja na kutoa huduma za viwango vya kimataifa katika utambuzi wa bidhaa, pia hutakiwa kusimamia na kuratibu mfumo wake na kuishauri sekta za biashara na viwanda katika matumizi yake," amefafanua Bi. Fatma.
Makamu mwenyekiti wa GS1 Hamad Hamad anayetokea Zanzibar amebainisha katika soko la ushindani wa kibiashara hivi sasa kila nchi inajitajidi kuwawekea mazingira rafiki wajasirimali wake ili kujiimarisha kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.
"Baada ya mafunzo haya nendeni mkafanye uchambuzi mzuri wa makundi ya bora ya wajasirimali na mtupatie ili tuweze kuwapa mbinu sahihi za kupiga hatua zaidi na hatimaye kulimidu soko la kimataifa," amesema Makamu Mwenyekiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.